Korea Kaskazini, China, Russia: Tuko pamoja na Iran
Nchi za Korea Kaskazini, China na Russia zimetangaza kuwa ziko pamoja na Iran katika mashambulizi ya jana Ijumaa ya Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Russia Today imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, serikali ya Korea Kaskazini imetangaza waziwazi kuwa iko pamoja na Iran kwa nguvu na hali zote.
Katika upande mwingine, na kwenye ujumbe uliosambazwa katika mtandao wa kijamii wa X kuhusu mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran, Rais Vladimir Putin wa Russia amesema wazi kuwa "Russia inaiunga mkono Iran."
Nayo Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesisitiza kwamba jamii ya kimataifa haiwezi kubakia kimya na kuangalia kwa macho tu jinai hizo za Israel zinazoharibu amani na kudhuru usalama wa kikanda na kimataifa.
Moscow, imeelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu kuongezeka hatari ya mivutano katika eneo la Asia Magharibi na kuongeza kuwa, ukweli ni kwamba mashambulizi ya Israel yamefanyika kwenye wakati ambao uko katikati baina ya mkutano wa Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA na kukaribia duru nyingine ya mazungumzo baina ya Iran na Marekani.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Hatua hiyo ya Israel imedhoofisha na kurudisha nyuma, juhudi za pande nyingi ambazo zilikuwa zinafanywa kwa taabu kupunguza uwezekano wa kutokea vita na kutafuta suluhu zinazoondoa shaka kuhusiana na nishati ya nyuklia ya Iran."
Naye msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ameeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran, akiilaani Israel kwa kutoheshimu mamlaka ya kujitawala ya Iran.