Sababu za India kupinga sera za kindumakuwili za EU ni zipi?
Wizara ya Mambo ya Nje ya India imepinga vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Russia na kiwanda cha kusafisha mafuta cha India na pia "sera za kindumakuwili" za umoja huo katika uga wa biashara ya nishati.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya India, Randhir Jaiswal, jana Ijumaa aliandika katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X kuhusu vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Russia kwamba: "India haiungi mkono vikwazo vyovyote vya upande mmoja. Sisi ni wchezaji tunaowajibika na tunaendelea kuheshimu kikamilifu majukumu yetu ya kisheria." Aliongeza kuwa: "Serikali ya India inautambua usalama wa nishati kuwa jukumu muhimu sana katika kukidhi mahitaji ya kimsingi ya raia wake. Tunasisitiza kwamba kusiwe na sera za kindumakuwili katika uwanja wa biashara ya nishati."
Umoja wa Ulaya siku ya Ijumaa uliidhinisha awamu ya 18 ya vikwazo dhidi ya Russia kutokana na vita vya Ukraine. Mojawapo ya vyombo vilivyowekewa vikwazo ni kiwanda cha kusafisha mafuta cha India kinachomilikiwa na kampuni ya Russia, Rosneft. Vikwazo hivyo, ambavyo viliidhinishwa na mabalozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels Ijumaa, Julai 18, ni pamoja na kupiga marufuku miamala na benki 22 za Russia, Mfuko wa Uwekezaji wa Moja kwa Moja wa Russia na kampuni zake tanzu, na marufuku ya kutumia moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja mabomba ya chini ya bahari ya Nord Stream.
Vikwazo hivyo vinapunguza bei ya kununua mafuta ya Russia katika Umoja wa Ulaya kutoka dola 60 hadi 47.6 kwa pipa, na kuweka vikwazo kwa meli 105 za mafuta ambazo EU inadai ni sehemu ya meli kivuli za Russia.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema siku ya Ijumaa akijibu vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Russia kwamba: "Tumesema mara kwa mara kwamba tunatambua vikwazo hivyo vya upande mmoja kuwa ni kinyume cha sheria na tunavipinga." Aliongeza kuwa: "Shirikisho la Russia limezoea kuishi chini ya vikwazo na limepata kinga makhsusi mkabala wa vikwazo."

Malalamiko ya India dhidi ya undumakuwili wa nchi za Magharibi hususan Umoja wa Ulaya kuhusiana na biashara ya nishati, kwa mara nyingine tena yamefichua unafiki na misimamo ya nchi za Magharibi katika nyanja mbalimbali hususan kuhusiana na nchi pinzani au mahasimu. Ulaya pamoja na Marekani, wamepitisha na kutekeleza maelfu ya vikwazo dhidi ya Russia tangu kuanza kwa vita vya Ukraine mnamo Februari 2022. Vikwazo hivi vinahusu nyanja mbalimbali za kiuchumi, kibiashara, kifedha, kisiasa, kidiplomasia na hata kimichezo. Licha ya vikwazo hivyo, nchi zisizo za Magharibi kama India, kwa kuzingatia maslahi ya kitaifa, zimejaribu kuendeleza biashara na miamala ya kifedha na Russia, haswa katika nyanja za usafirishaji wa nishati, yaani mafuta na gesi, na zimeendelea kuagiza mafuta kutoka Russia licha ya mashinikizo la Magharibi. Hii ni pamoja na kwamba licha ya Umoja wa Ulaya kuwekea vikwazo vya nishati dhidi ya Russia, baadhi ya nchi za umoja huo kama Hungary na Slovakia zimeendelea kuagiza mafuta na gesi kutoka Urusi baada ya kupata misamaha.
Kutokana na hali hiyo, Umoja wa Ulaya pamoja na Marekani, zimetekeleza misamaha mbalimbali kwa wanachama wake, huku zikitoa shinikizo kubwa kwa nchi nyingine kutonunua mafuta na gesi kutoka Russia. Kwa utaratibu huo Umoja wa Ulaya pamoja na Marekani, zimetoaa misamaha kwa wanachama na washirika wao, huku zikizidisha mashinikizo makubwa kwa nchi nyingine ya kutonunua mafuta na gesi kutoka Russia. Hii ndio sera ya kinafiki na kindumakuwili ya Umoja wa Ulaya katika uwanja wa biashara ya nishati ambayo India imeipinga vikali kwa kuzingatia duru mpya ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Russia.
Muhimu ni kwamba, suala la sera za kinafiki na kindumakuwili za Magharibi ni msingi wa kuelewa ni kwa nini nchi nyingi za kusini mwa dunia, ikiwa ni pamoja na India, zimekataa kukubaliana na vikwazo vya Magharibi dhidi ya Russia baada ya vita vya Ukraine. Mashambulio ya NATO dhidi ya Serbia mwaka 1999 na uvamizi ulioongozwa na Marekani nchini Iraq mwaka 2003, yote mawili yalifanywa bila ya kibali cha Umoja wa Mataifa, na vilevile kufumbiwa macho kwa miongo kadhaa kwa jinai za Israel dhidi ya Wapalestina, hususan mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni huko Gaza, kunazifanya nchi za Kusini mwa dunia kuzikosoa vikali nchi za Magharibi kutokana na misimamo yao ya kinafiki na kindumakuwili kuhusu masuala mbalimbali kama ugaidi, vikwazo na haki za binadamu.