UN: Mzozo wa Rohingya umezidi kuwa mbaya kwa zaidi ya miaka minane sasa
Miaka minane baada ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Mynmar kulazimika kuhama katika Jimbo la Rakhine, Umoja wa Mataifa umesema kuwa mzozo unaowakabili raia hao umezidi kuwa mbaya.
Jeremy Laurence, msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) ametaka kukomeshwa ukatili na ukandamizaji dhidi ya watu wa kabila la Rohingya huko Myanmar.
Itakumbukwa kuwa watu milioni moja miongoni mwa jamii ya Waislamu walio wachache wa Rohingya walikimbia mashambulizi yaliyoanzishwa na jeshi la Mynamar tarehe 25 Agosti 2017, kampeni ambayo wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wameitaka kuwa ni "kielelezo cha maangamizi ya kizazi".
Jeshi la Myanmar liliitaja kampeni yake hiyo kuwa ni halali ya kupambana na ugaidi.
Zaidi ya Warohingya milioni moja walivuka mpaka na kuingia Bangladesh ambako wanaendelea kuishi hadi sasa katika kambi zisizofaa wakiwa na matarajio madogo ya kurejea nyumbani. Aghalabu ya Waislamu hao wamenyima uraia na haki nyingine za msingi huko Bangladesh.

Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa tangu mwishoni mwaka mwaka 2023 watu wengi zaidi walilikimbia jimbo la Rakhine, magharibi mwa Myanmar, kutokana na kuongezeka mapigano kati ya jeshi la nchi hiyo na wapiganaji wa Arakan. Jeshi la Arakan linaundwa na wanamgambo wa kikabila.