Dec 28, 2022 08:01 UTC
  • Umoja wa Mataifa waomba misaada kwa ajili wakimbizi wa Rohingya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi limeziomba msaada kwa nchi mbalimbali kwa ajili ya wakimbizi wa Rohingya baada ya Waislamu wasiopungua 20 wa jamii hiyo kuaga dunia baharini na mamia ya wengine kunusurika kifo katika ufuo wa Indonesia baada ya wiki kadhaa za kutangatanga katika Bahari ya Hindi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi limetangaza kuwa karibu Warohingya 500 wamewasili Indonesia katika muda wa wiki sita zilizopita.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeutaja mwaka unaomalizika wa 2022 kuwa kati ya miaka mibaya zaidi kwa Warohingya ambao wengi wao wameaga dunia baharini wakikimbia hali mbaya ya kambi za wakimbizi huko Bangladesh.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamesema kuwa mashua iliyokuwa imebeba wakimbizi 180 kwa Kirohingya ilizama baharini mapema mwezi huu wa Disemba na kwamba watu wote waliokuwemo wanaaminika kufamaji.

Itakumbukwa kuwa, Agosti 2017, zaidi ya Waislamu laki saba wa jamii ya Rohingya walilazimika kuhama makazi yao nchini Myanmar na kukimbilia kwenye kambi za wakimbizi nchini Bangladesh ili kutafuta hifadhi na kunusuru maisha yao, baada ya jeshi la Myanmar, likishirikiana na Mabudha wenye chuki za kidini, kuanzisha operesheni ya kuwaondoa kwa nguvu Waislamu hao kwa kisingizio cha mashambulizi yaliyofanywa na kundi moja la waasi. Vikosi vya jeshi la Myanmar vimehusika na jinai mbalimbali dhidi ya Waislamu Warohingya zikiwemo za ubakaji wa halaiki, mauaji na kuchoma moto maelfu ya nyumba zao.

Tags