Ufaransa 'yamjia juu' balozi wa US Paris kwa kuituhumu kuwa inahatarisha maisha ya Mayahudi
Ufaransa imemwita balozi wa Marekani nchini humo Charles Kushner, baada ya mwanadiplomasia huyo kumwandikia barua Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa akidai kwamba Paris imeshindwa kuchukua hatua za kutosha kukomesha vitendo vya mabavu dhidi ya Mayahudi raia wa nchi hiyo.
Kushner aliandika barua hiyo ya wazi katika toleo la jana Jumapili la Jarida la Wall Street, akielekeza shutuma kwa ukosoaji inaofanya Ufaransa dhidi ya utawala wa kizayuni wa Israel unaolaaniwa kila pembe ya dunia kwa mauaji ya kimbari ya Wapalestina wa Ghaza.
Aidha ameikosoa vikali Paris kwa kutangaza kuwa italitambua taifa la Palestina.
Kushner, ambaye ni baba wa Jared ambaye ni mkwe wa rais wa Marekani, ameeleza katika barua yake kwa Rais wa Ufaransa: "taarifa za umma zinazoisumbua Israel na dalili za kutambuliwa taifa la Palestina zinawatia moyo watu wenye msimamo mkali, kuchochea ghasia na kuhatarisha maisha ya Wayahudi nchini Ufaransa. Katika ulimwengu wa leo, chuki dhidi ya Uzayuni ni sawa na chuki dhidi ya Uyahudi, hilo liko wazi na rahisi kabisa".
Kufuatia tuhuma hizo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imemwita balozi huyo wa Marekani, sambamba na kueleza katika taarifa: "Ufaransa inakanusha vikali madai haya ya hivi punde. Madai kutoka kwa balozi hayakubaliki".
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Paris "imejitolea kikamilifu" kupambana na chuki dhidi ya Wayahudi na kwamba maoni ya Kushner yanakwenda "kinyume na sheria za kimataifa, hususan jukumu la wafanyakazi wa kidiplomasia kutoingilia masuala ya ndani ya mataifa".
Wakati huohuo Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetoa taarifa na kusema, inasimama na maoni yaliyotolewa na balozi wake.
"Balozi Kushner ni mwakilishi wetu wa serikali ya Marekani nchini Ufaransa na anafanya kazi nzuri kuendeleza maslahi yetu ya kitaifa katika jukumu hilo," ameeleza msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Tommy Pigott katika taarifa hiyo.../