EU yasisitiza kuiunga mkono "kwa dhati" ICC baada ya US kuwawekea vikwazo waendesha mashtaka 2
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema "amesikitishwa sana" na uamuzi wa Marekani wa kuwawekea vikwazo maafisa wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).
Kaja Kallas ameyasema hayo katika taarifa iliyotolewa na idara ya Huduma ya Nje ya Ulaya (EEAS) ambayo ni kitengo cha kidiplomasia cha EU na kusisitiza: "kwa mara nyingine tena EU inaeleza ilivyosikitishwa sana na uamuzi wa kuwawekea vikwazo manaibu Waendesha Mashtaka wawili na majaji wawili wa ICC. Uamuzi huu unaweza kuathiri utendaji wa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka na uchunguzi unaoendelea".
Kallas amesisitiza katika taarifa yake juu ya "uungaji mkono wa dhati" wa EU kwa ICC, akiahidi "msaada na mchango" zaidi ili kuhakikisha ulinzi wa Mahakama hiyo na wafanyakazi wake dhidi ya shinikizo au vitisho kutoka nje.
"Mashambulizi au vitisho dhidi ya Mahakama, viongozi waliochaguliwa, wafanyakazi na wale wanaoshirikiana na Mahakama hayakubaliki. ICC lazima iwe na uwezo wa kufanya kazi kwa uhuru na bila upendeleo," imeongezea kueleza taarifa hiyo ya mkuu wa sera za nje wa EU.
Aidha, Kallas ametoa wito kwa mataifa yote kuhakikisha yanatoa "ushirikiano kamili" kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, "ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa haraka wa hati za kukamatwa ambazo hazijakamilika, na kuingia katika mikataba ya hiari."
Vikwazo vya karibuni zaidi vya Marekani dhidi ya ICC ni vile vilivyotangazwa siku ya Jumatano viliwalenga majaji wawili wa mahakama hiyo na manaibu waendesha mashtaka wawili. Vikwazo hivyo vinafanana na walivyowekewa majaji wanne mwezi Juni na mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo ya kimataifa mapema mwaka huu.../