Je, kustawishwa ushirikiano wa Russia na India ni jibu kwa sera ya mashinikizo ya Trump?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130028-je_kustawishwa_ushirikiano_wa_russia_na_india_ni_jibu_kwa_sera_ya_mashinikizo_ya_trump
Sambamba na mashinikizo ya utawala wa Trump dhidi ya India ili ipunguze uhusiano wake na Russia, Waziri wa Mambo ya Nje wa India alisafiri hadi Moscow na kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Russia Vladimir Putin.
(last modified 2025-08-27T02:21:42+00:00 )
Aug 27, 2025 02:21 UTC
  • Je, kustawishwa ushirikiano wa Russia na India ni jibu kwa sera ya mashinikizo ya Trump?

Sambamba na mashinikizo ya utawala wa Trump dhidi ya India ili ipunguze uhusiano wake na Russia, Waziri wa Mambo ya Nje wa India alisafiri hadi Moscow na kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Russia Vladimir Putin.

Mnamo Agosti 21, Putin alikutana na Subrahmanyam Jaishankar, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya India na Mwenyekiti wa upande wa India wa Tume ya Kiserikali ya Russia-India ya Biashara, Uchumi, Sayansi, Ushirikiano wa Kiufundi na Kitamaduni.

Siku moja kabla, Jaishankar na Manturov walikuwa wameitisha kikao cha tume ya pamoja ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili huko Moscow. Baada ya mkutano huo, Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Russia alisema: "Mauzo ya biashara kati ya Russia na India yameongezeka karibu mara saba katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. India ni kati ya washirika watatu wakubwa wa biashara ya nje wa Russia.

Zaidi ya asilimia 90 ya biashara kati ya Russia na India inafanywa kwa kutumia sarafu za kitaifa," Manturov alibainisha. "Russia na India zinakusudia kuendeleza kwa pamoja Njia ya Bahari ya Kaskazini na ukanda wa usafiri wa Kaskazini-Kusini. Tunatumai kwamba ushirikiano kati ya Russia na India katika nyanja ya nishati ya nyuklia ya amani utapanuka, ikiwa ni pamoja na kwa msingi wa uzoefu wa mafanikio wa mradi wa kinu cha nyuklia cha Koodankulam."

Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa India na Russia

 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov pia alisisitiza wakati wa mazungumzo baina na Waziri mwenzake wa Mashauri ya Kigeni wa India kkwamba: "Katika hali ya sasa, maingiliano yetu katika jukwaa la kimataifa yanapata umuhimu, hasa kwa kuundwa kwa usanifu mpya, wenye lengo la pande nyingi. Katika ukweli huu mpya, vikao kama vile Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, BRICS na G20 vinachukua nafasi inayoongezeka."

Waziri wa Mambo ya Nje wa India ameashiria pia vitisho na mashinikizo makubwa ya Washington dhidi ya New Delhi kwa kisingizio cha India kununua mafuta ya Russia na kusema: "India inashangazwa na mantiki ya Marekani kuishutumu New Delhi kwa kununua mafuta kutoka Russia, kwa sababu hapo awali Washington ilisisitiza kudumisha utulivu katika masoko ya kimataifa."

Matamshi ya afisa huyu wa India kwa mara nyingine tena yanaonyesha waziwazi sera za kindumakuwili za Washington mkabala wa sera ya kimataifa ya nishati, pamoja na mbinu ya Marekani ya kivita na uonevu katika maingiliano na nchi nyingine.

Ukweli ni kwamba licha ya shinikizo la kila upande kutoka kwa Marekani, ikiwa ni pamoja na kutoza ushuru wa asilimia 50 kwa bidhaa zinazosafirishwa kwenda Marekani kutokana na kuendelea kununua mafuta kutoka Russia, India imeendelea kutilia mkazo kupanua uhusiano wake na Moscow katika nyanja mbalimbali na haijakubali kusalimu amri mbele ya ubabe wa Washington.

Kwa ujumla, ushahidi unaonyesha kwamba kupanuliwa ushirikiano wa Russia na India kumekuwa kwa kiasi kikubwa ni jibu la kimkakati kwa sera za utawala wa Trump za shinikizo na ushuru mkubwa. Muktadha wa ushirikiano huu na sababu zake zinaweza kufupishwa kama ifuatavyo:

-        Kuongeza ushuru wa Marekani kwa bidhaa za India: Utawala wa Trump uliongeza ushuru wa forodha kwa bidhaa zilizoagizwa kutoka India kwa 50%, jambo ambalo lilisababisha mvutano wa kibiashara na kuisukuma India kuimarisha uhusiano na wapinzani wa Washington, haswa Russia na China.

-        Upinzani wa India dhidi ya shinikizo la Washington: New Delhi sio tu haikurudi nyuma, lakini pia ilipanua uhusiano wake wa kiuchumi na Russia na China kwa kasi ya haraka. Hatua hii inaonyesha azma ya India ya kudumisha uhuru wake wa kidiplomasia na kiuchumi.

Rais Donald Trump wa Marekani

 

-        Kununua mafuta kutoka Urusi: India ni mmoja wa wanunuzi wakubwa wa mafuta ya Russia. Marekani imeona manunuzi haya kama kufadhili vita nchini Ukrraine na imejaribu kutumia shinikizo la kiuchumi kuiondoa India kutoka kwa njia hii. Hata hivyo, India imekataa dai hili na kulichukulia kuwa ni mfano wa "undumakuwili" wa Magharibi.

-        Kuendeleza ushirikiano wa nishati na usafiri: Russia na India zina miradi ya pamoja katika sekta ya nishati, ikiwa ni pamoja na uchimbaji wa rasilimali katika eneo la Arctic na maendeleo ya ukanda wa usafiri wa Kaskazini-Kusini.

Kwa ujumla, inaonekana kwamba kustawishwa uhusiano wa India-Russia kunaweza kuchukuliwa kuwa sehemu ya diplomasia yenye uwiano inayolenga kupunguza utegemezi kwa nchi za Magharibi na kukabiliana na siasa za upande mmoja za Marekani hususan katika zama za Trump.

Ushirikiano huu sio tu unapanuka katika nyanja ya uchumi, lakini pia una ujumbe muhimu wa kijiopolitiki, ambao ni kusisitiza juuu ya kuweko kambi kadhaa katika mfuumo wa kimataifa na kupungua kwa ushawishi wa Washington katika Asia.