Trump dhidi ya Modi: Ni nini matokeo ya kuanza rasmi vita vya ushuru vya Marekani dhidi ya India?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130114-trump_dhidi_ya_modi_ni_nini_matokeo_ya_kuanza_rasmi_vita_vya_ushuru_vya_marekani_dhidi_ya_india
Marekani imeanza kutekeleza ushuru wa asilimia 50 kwa bidhaa zinazoingizwa nchini humo kutoka India.
(last modified 2025-08-28T10:46:04+00:00 )
Aug 28, 2025 10:46 UTC
  • Trump dhidi ya Modi: Ni nini matokeo ya kuanza rasmi vita vya ushuru vya Marekani dhidi ya India?

Marekani imeanza kutekeleza ushuru wa asilimia 50 kwa bidhaa zinazoingizwa nchini humo kutoka India.

Serikali ya Marekani, kwa amri ya rais wa nchi hiyo, ilianza kutekeleza ushuru wa takriban 50% kwa bidhaa zote zinazoagizwa kutoka India kuanzia Jumatano, Agosti 27; nusu ya kiasi hiki imetangazwa kama "adhabu" kwa sababu ya India kununua mafuta kutoka Russia. Utekelezaji kamili wa ushuru mpya dhidi ya India una maana ya kutumia sera ya biashara kama wenzo kwa ajili ya malengo ambayo ni zaidi ya masuala ya biashara, ikiwa ni pamoja na kuweka mashinikizo kwa nchi zinazofanya biashara ya nishati na Russia.

Kwa kutekeleza ushuru wa asilimia 50 kwa bidhaa kutoka India, Washington imetekeleza mojawapo ya hatua zake kali za ushuru dhidi ya nchi yenye uhusiano mkubwa wa kiuchumi na Marekani. Uamuzi huo, kama wasemavyo wachambuzi wa mambo, unahatarisha kuathiri mauzo ya bidhaa za India nje ya nchi (kuanzia dawa na vito hadi nguo na mashine) na kudhoofisha uwekezaji wa kigeni katika soko la hisa la nchi hiyo. Kuongezeka kwa ushuru dhidi ya India kunaweza kudhoofisha mkakati wa waagizaji wa Marekani katika miaka ya hivi karibuni wa kuhamisha uzalishaji kutoka China hadi India.

Trump na Modi

India, sasa imekuwa mlengwa mkuu wa vita vya ushuru vya Trump baada ya Marekani kuiwekea nchi hiyo ushuru wa juu zaidi wa asilimia 50. Hatua hiyo ya Marekani imekabiliwa na msimamo mkali kutoka India na imeongeza kwa kiasi kikubwa mvutano kati ya Washington na New Delhi. John Bolton, mshauri wa zamani wa Usalama wa Taifa wa Merekani katika muhula wa kwanza wa Donald Trump, anaamini kwamba India inahisi "vibaya sana" kwa kuwa lengo na shabaha ya vitisho vya ushuru na vikwazo vya Trump, wakati Russia na Uchina zinakabiliwa na mashinikizo madogo. Bolton ameongeza kuwa: "Kadiri India inavyotengwa, ndivyo uhusiano kati ya New Delhi na Washington unavyozidi kuwa mbaya zaidi."

Kuhusiana na suala hili, ripoti zinasema kuwa, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi amekataa kujibu simu za Rais wa Marekani, Donald Trump mara nne katika wiki za hivi karibuni. Uhusiano wa Marekani na India unaonekana kudorora baada ya hapo awali kuelezwa na serikali zote mbili kama "ushirikiano muhimu zaidi wa karne ya 21." Inaonekana kwamba Trump amekuwa akitafuta suluhisho la kupunguza mvutano, lakini kukataa kwa Modi kuzungumza naye kumemkasirisha. Baadhi wanasema, kitendo cha Modi cha kukataa kuzungumza na Trump kinahusiana na wasiwasi kuhusu uwezekano wa Rais wa Marekani kupotosha matokeo ya mazungumzo hayo hasa kuhusu suala nyeti la uhusiano wa India na Pakistan. Trump amekuwa akidai mara kwa mara kwamba alizuia mzozo wa nyuklia kati ya India na Pakistan kwa kutumia mashinikizo ya kibiashara, madai ambayo serikali ya India imeyakanusha.

Ushuru mpya wa Marekani dhidi ya India pia una athari kubwa za kisiasa ndani ya India. Bila kutaja moja kwa moja jina la Trump au nyongeza ya ushuru, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi ametaja kipaumbele chake kuwa ni "kusaidia biashara ndogo ndogo, wauzaji wa madukani na wakulima" na kusema, "India itaibuka na ushindi licha ya mashinikizo yaliyopo." Vilevile ameashiria uwezekano wa kutazamwa upya uhusiano wa kiuchumi wa India na kuwa na washirika tofauti kuanzia China, Japan hadi Ulaya. Matamshi haya ni ishara ya azma ya India la kukabiliana na mashinikizo ya ushuru ya Marekani na kujaribu kupanga upya uhusiano wake na mataifa mengine makubwa ya kiuchumi duniani, hasa China na Umoja wa Ulaya, na maeneo muhimu kama vile Asia Mashariki, Asia Magharibi, pamoja na Amerika Kusini.

Mabadiliko hayo pia yanatoa changamoto kwa uhusiano ambao umejengwa kwa zaidi ya miaka 25 kwa diplomasia amilifu ya pande zote mbili, na kwa uwepo mkubwa wa makampuni ya Marekani nchini India.

Sasa, India pamoja na Brazili, ni miongoni mwa nchi chache zinazokabiliwa na ushuru wa forodha wa asilimia 50, kiwango ambacho ni cha juu zaidi kuliko washindani wengine katika bara Asia. Jambo hili linaweza kuongeza gharama za uagizaji na hatari ya upangaji wa ugavi kwa makampuni ya Marekani ambayo yalikuwa yakiitazama India kama mbadala wa Uchina.

Hata hivyo, sio tu kwamba India haijalegeza kamba mbele ya mashinikizo ya Marekani, lakini pia imepanua uhusiano wake wa kiuchumi na Russia na Uchina kwa haraka na kasi kubwa. Hatua hii inaonyesha azma ya India ya kudumisha uhuru na kujitegemea kwake kidiplomasia na kiuchumi.