Russia: Tumepiga Ukraine kwa makombora ya hypersonic
Russia imetangaza habari ya kutekeleza mashambulizi ya masafa marefu dhidi ya shabaha za jeshi la Ukraine, kwa kutumia aina mbalimbali za silaha, yakiwemo makombora ya hypersonic aina ya Kinzhal.
Wizara ya Ulinzi ya Moscow iliripoti hayo jana Alkhamisi na kueleza kuwa, katika operesheni hiyo, makombora ya Russia yalilenga mitambo kadhaa ya silaha na viwanja vya ndege za kijeshi vya Ukraine.
Jeshi la Ukraine limedai kuwa lilitungua ndege nyingi zisizo na rubani na makombora yaliyovurumishwa, lakini limekiri kufanikiwa kwa mashambulizi ya Russia katika maeneo 13.
Moja ya mashambulio hayo lilinaswa kwenye kamera za CCTV, huku picha zilizosambaa mitandaoni zikionyesha makombora mawili yakipiga eneo moja katikati mwa Kiev.
Igor Zinkevich, mjumbe wa baraza la jiji la Lviv, amedai kuwa Russia pia ilipiga kituo cha kijeshi huko Kiev unaoendeshwa na kampuni ya kijeshi ya Uturuki ya Bayraktar, na kuongeza kuwa shambulio hilo lilikuwa la nne la aina yake katika kipindi cha miezi sita.
Wiki iliyopita, vyombo vya habari vya Ukraine viliripoti shambulio la kombora la cruise linaloitwa Flamingo, lenye uwezo kupiga umbali wa kilomita 3,000 na uzani wa hadi kilo 1,000.
Kabla ya hapo pia, vikosi vya ulinzi wa anga vya Russia viliitungua ndege isiyo na rubani ya Ukraine (droni) iliyokuwa imekusudia kutekeleza shambulizi katika kiwanda cha nguvu za nyuklia cha Kursk cha Russia (KNPP).