Trump afufua tena simulizi za 'Riviera' ya Ghaza katika mkutano na Blair na Kushner
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130144-trump_afufua_tena_simulizi_za_'riviera'_ya_ghaza_katika_mkutano_na_blair_na_kushner
Rais Donald Trump wa Marekani amefufua tena mpango wake wa kuwahamisha Wapalestina wote katika Ukanda wa Ghaza na kuligeuza eneo hilo la ardhi ya Palestina kuwa sehemu ya starehe na burudani alipokutana ikulu ya White House na mkwewe Jared Kushner na waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair ambao wote wawili wanahusishwa na uandaaji wa mpango huo unaotajwa kuwa ni wa kikoloni.
(last modified 2025-10-22T06:10:45+00:00 )
Aug 29, 2025 07:33 UTC
  • Trump afufua tena simulizi za 'Riviera' ya Ghaza katika mkutano na Blair na Kushner

Rais Donald Trump wa Marekani amefufua tena mpango wake wa kuwahamisha Wapalestina wote katika Ukanda wa Ghaza na kuligeuza eneo hilo la ardhi ya Palestina kuwa sehemu ya starehe na burudani alipokutana ikulu ya White House na mkwewe Jared Kushner na waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair ambao wote wawili wanahusishwa na uandaaji wa mpango huo unaotajwa kuwa ni wa kikoloni.

Blair ameshiriki katika mkutano huo wa White House ulioongozwa na Trump na Kushner kujadili mustakabali wa Ghaza, mkutano ambao umeibua wasiwasi kutokana na kuwatenga Wapalestina na mpango huo ambao wengi wanauelezea kama ramani ya ufutaji wa kizazi cha Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.

Mkutano huo, ulioelezewa na mjumbe wa Trump katika Mashariki ya Kati Steve Witkoff kama "mkusanyiko mkubwa" umeripotiwa kuwa umezingatia hali ya Ghaza baada ya vita ambayo inaangazia utekelezaji wa wito uliotolewa huko nyuma na rais wa Marekani wa kuwahamisha watu wote wa eneo hilo lililowekewa mzingiro na kulibadilisha kuwa sehemu ya burudani na starehe yaani "Riviera" inayodhibitiwa na Marekani katika Bahari ya Mediterania.

Maono hayo ya kuigeuza Ghaza "Riviera" yamelaaniwa vikali na mashirika ya kiraia ya Palestina, wasomi wa sheria wa kimataifa na mashirika mengi ya haki za binadamu ambayo yameyaelezea kama njozi hatari inayotokana na mantiki ya kikoloni.

Mkutano wa White House umefanyika wakati jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel linajitayarisha kufanya mashambulizi mapya ya ardhini katika Jiji la Ghaza, na baada ya harakati ya Hamas kukubali mpango wa kusitisha mapigano ambao Israel imeukataa licha ya kuwa iliukubali hapo kabla. Sambamba na hilo, maafisa wa serikali ya Trump wanaendesha kampeni ya kuzuia mipango ya kutambuliwa taifa huru la Palestina katika Umoja wa Mataifa, na kuwashinikiza washirika wake ikiwa ni pamoja na Uingereza, Ufaransa na Australia waungane na kampeni hiyo ya Washington…/