Kwa nini zaidi ya wanadiplomasia 200 wa Ulaya wanaukosoa Umoja wa Ulaya kwa kutochukua hatua kuhusu vita vya Gaza?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130152-kwa_nini_zaidi_ya_wanadiplomasia_200_wa_ulaya_wanaukosoa_umoja_wa_ulaya_kwa_kutochukua_hatua_kuhusu_vita_vya_gaza
Idadi kubwa ya wanadiplomasia wakuu wa zamani wa Ulaya wametaka Umoja wa Ulaya au nchi wanachama wachukue hatua za haraka kuhusiana na vita vya utawala wa Kizayuni huko Gaza na hatua zake zilizo kinyume cha sheria katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
(last modified 2025-08-29T10:03:05+00:00 )
Aug 29, 2025 10:03 UTC
  • Kwa nini zaidi ya wanadiplomasia 200 wa Ulaya wanaukosoa Umoja wa Ulaya kwa kutochukua hatua kuhusu vita vya Gaza?

Idadi kubwa ya wanadiplomasia wakuu wa zamani wa Ulaya wametaka Umoja wa Ulaya au nchi wanachama wachukue hatua za haraka kuhusiana na vita vya utawala wa Kizayuni huko Gaza na hatua zake zilizo kinyume cha sheria katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Zaidi ya wanadiplomasia 200 waandamizi wa Ulaya katika barua ya wazi iliyotumwa kwa maafisa wa umoja huo wametaka kuchukuliwa hatua za haraka dhidi ya utawala wa Kizayuni ili kusimamisha vita vya Gaza na vitendo vyake haramu katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Barua hii imetiwa saini na wawakilishi pamoja na mabalozi wa zamani 209 wa nchi za Ulaya. Waliotia saini barua hiyo ni pamoja na mabalozi 110 wa zamani, wakurugenzi wakuu 25 wa zamani, na Alain Le Roi, katibu mkuu wa zamani wa huduma za nje wa Umoja wa Ulaya, na vile vile Carlo Trojan, katibu mkuu wa zamani wa Tume ya Ulaya.

Barua hii, inasisitizwa kuwa ikiwa Umoja wa Ulaya hauwezi kuchukua hatua kwa pamoja kuhusu suala hili, nchi wanachama zinapaswa kuchukua hatua kivyake au kwa namna ya vikundi vidogo ili kulinda haki za binadamu na kutekeleza sheria za kimataifa.

Wanadiplomasia hao wamependekeza mbinu tisa zichukuliwe katika barua hii; ikiwa ni pamoja na kusimamisha leseni za kuuza silaha nje ya nchi, kupiga marufuku biashara ya bidhaa na huduma, na vitongoji haramu, na kuzuia vituo vya data vya Ulaya kusindika au kuhifadhi data za serikali au kampuni za Israel zilizopo katika Gaza na maeneo mengine yanayokaliwa kwa mabavu.

Esson Cohen van Borgsdorff, mwakilishi wa zamani wa Umoja wa Ulaya huko Palestina na mmoja wa waratibu wa mpango huu amesema: "Taasisi za Ulaya zinakabiliwa na ongezeko la kukatisha tamaa na haziwezi tena kukaa kimya mbele ya utepetevu wa nchi 27. Hii ina maana ya kusaliti maadili yetu." Ameongeza: "Serikali za Ulaya zinapoteza imani sio kusini mwa ulimwengu tu, bali pia na raia wao zenyeywe." Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya haujaweza kutoa uungaji mkono wa dhabiti kwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ wala Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC katika kufuatilia jinai za kivita huko Gaza.

Kutochukua hatua Umoja wa Ulaya kuhusiana na vita vya Gaza na sasa hatua mpya za Israel katika Ukingo wa Magharibi ni suala ambalo limekosolewa vikali na maafisa wa zamani, taasisi za Ulaya na mashirika ya kutetea haki za binadamu. Zifuatazo ni baadhi ya sababu za umoja huo kutochukua hatua katika uwanja huo.

Sababu za kisiasa na kidiplomasia

- Utegemezi kwa Marekani na Israel: Nchi nyingi wanachama wa EU zina uhusiano wa karibu wa kisiasa, kiuchumi na kiusalama na Marekani na Israel, jambo ambalo linazizuia kuchukua misimamo madhubuti dhidi ya hatua za Israel huko Gaza.

- Mgongano wa maslahi ya ndani: Kutoelewana kati ya nchi wanachama wa EU kuhusu namna ya kukabiliana na mgogoro wa Gaza kumeufanya umoja huu kushindwa kufikia makubaliano na kuchukua hatua madhubuti. Nchi kama Uhispania, Ireland na Slovenia zina misimamo muhimu kuhusu Israel, huku Hungary, Jamhuri ya Czech na Ujerumani zikiwa washirika wa karibu wa utawala huo haramu. 

Watoto wenye njaa huko Gaza

Sera ya mambo ya nje ya Umoja wa Ulaya inahitaji makubaliano ya pamoja, suala ambalo limezuia kuchukuliwa hatua madhubuti kama vile vikwazo au kusitishwa makubaliano ya biashara na Israel.

Udhaifu katika kutumia zana za mashinikizo

- Kutosimamishwa kwa mikataba ya biashara: Licha ya maombi mengi ya kusimamisha makubaliano ya ushirikiano na Israel, Umoja wa Ulaya kwa muda mrefu ulikataa kuchukua hatua yoyote, na kupendekeza tu kupitia upya makubaliano hayo, tena baada ya kupita miezi mingi baada ya kuanza vita, jambo ambalo nalo halikufikia popote kutokana na upinzani wa nchi zisizopungua 10 za Ulaya.

- Kushindwa kusitisha uuzaji wa silaha nje ya nchi: Baadhi ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, hasa Ujerumani, zimeendelea kuipa silaha Israel, wakati suala hili lingeweza kutumika kama chombo cha mashinikizo.

Ukosefu wa moyo wa kimaadili na kibinadamu

- Kuporomoka kwa itibari ya kimaadili: Josep Borrell, afisa wa zamani wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, amesema kwamba Umoja wa Ulaya umepoteza moyo na kwamba sasa unakabiliwa na kuporomoka kwa itibari yake ya kimataifa.

- Undumakuwili: Baadhi ya nchi za Ulaya, kama Hungary, zimemkaribisha nchini humo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, huku akisakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, na tabia hii inachukuliwa kuwa ya undumakuwili.

Wakati huo huo, sera za ndani za nchi za Ulaya zina nafasi muhimu katika kuimarisha nafasi ya Umoja wa Ulaya kuhusu vita vya Gaza. Sera hizi haziathiri tu maamuzi ya kidiplomasia, bali wakati mwingine huzuia hatua madhubuti kuchukuliwa dhidi ya Israel. Sababu zifuatazo zinaweza kuorodheshwa katika muktadha huu:

Migogoro ya ndani ya serikali na bunge

- Ukosefu wa maafikiano katika baraza la mawaziri: Katika nchi kama Uholanzi, jaribio la waziri wa mambo ya nje la kuweka vikwazo dhidi ya Israel lilikabiliwa na upinzani mkali ndani ya serikali na hatimaye kumpelekea kujiuzulu.

- Mgogoro wa vyama vya siasa: Vyama vya kihafidhina kwa kawaida vinaunga mkono Israel, huku vyama vya mrengo wa kushoto vikitaka kusitishwa uuzaji silaha na kuwaunga mkono Wapalestina.

Maslahi ya kiuchumi na lobi zenye nguvu

- Uuzaji wa silaha na teknolojia nje ya nchi: Baadhi ya nchi, kama vile Ujerumani na Italia, zimekataa kusitisha ushirikiano wa kijeshi na Israel, kwa sababu mahusiano haya yana faida kubwa.

- Ushawishi wa lobi za Kizayuni: Lobi hizi zina ushawishi mkubwa katika baadhi ya nchi kama vile Ufaransa na Ujerumani na huzuia kupitishwa kwa sera dhidi ya Israel.

Mtazamo wa kihistoria na kitamaduni

- Madai ya mauaji ya Holocaust: Huko Ujerumani, uungaji mkono kwa Israel na serikali ya utawala huo unazingatiwa kama aina ya fidia ya kihistoria kwa tukio la Holocaust, ambapo ukosoaji wowote kuhusu suala hilo hukabiliwa na hatua kali, na uteteaji wowote kwa Wapalestina hupingwa bila kusita.

Kuhusu suala hili, Friedrich Mertes, Kansela wa Ujerumani amesisitiza kwamba Ujerumani, tofauti na nchi kama Kanada au Ufaransa, haitatambua "taifa la Palestina" wakati huu. Wakati huo huo, kura za maoni nchini Ujerumani zinaonyesha kuwa asilimia 80 ya watu wanapinga vitendo vya Israel huko Gaza, na thuluthi mbili wanataka serikali ichukue hatua.

- Ubaguzi wa Kimuundo: Baadhi ya wachambuzi wanaamini kwamba upuuzaji wa Ulaya kuhusu mateso ya Wapalestina unatokana na ubaguzi wa kimuundo na fikra za kikoloni.