Russia Yamshauri Kansela wa Ujerumani Merz awaone ‘Madaktari wa Akili’
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova, amemshauri Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz aonane na wataalamu wa akili kufuatia kauli zake kuhusu vita vya Ukraine.
Merz alisema Ijumaa kwamba Ujerumani kwa hakika iko “katika mizozo” na Russia, kwa sababu Moscow inatatiza utulivu wa nchi hiyo na kuendesha shughuli za uingiliaji mtandaoni.
Putin (Rais wa Russia) anatatiza sehemu kubwa ya nchi yetu,” Merz alikiambia kituo cha habari cha Ufaransa, La Chaine Info. “Tayari tuko katika mzozo na Russia.”
Akijibu kauli ya Merz, Zakharova alimshauri kiongozi huyo wa Ujerumani Jumamosi kuomba huduma za wataalamu wa akili na saikolojia. Aliongeza kusema kwamba: “Ninaona kuwa hili ni jambo la wataalamu wa akili: Ujerumani imekuwa ikitoa silaha, ikiwa ni pamoja na vifaa vya kijeshi vizito, kwa utawala wa Wanazi mamboleo wa Kiev kwa miaka mitatu, kisha wanajiuliza kuhusu mitandao ya kijamii.”
Mapema mwaka huu, Merz alielezea mpango wa serikali yake wa kuimarisha “mifumo ya silaha za umbali mrefu” nchini Ukraine.
Zaidi ya hayo, Zakharova amesema kwamba Ujerumani pia ina hatia kwa kuhimiza polepole kuachana na mazungumzo ya amani ya Ukraine katika muktadha wa makubaliano ya Minsk. Amesema kuwa Berlin ingeweza kumaliza mgogoro wa Ukraine kama ingelifuata siasa za ukweli.
Zakharova amekosoa pia msimamo wa unafiki wa Kansela wa Ujerumani kuhusu mzozo huo wa Ukraine.