Maduro aonya: Tutaingia kwenye ‘mapambano ya silaha’ ikiwa tutashambuliwa na US
Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro ameonya kwamba nchi yake itagura kutoka kwenye siasa na kuingia kwenye "mapambano ya kutumia silaha" iwapo Marekani itaanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya taifa hilo.
"Venezuela daima imekuwa tayari kuzungumza, kushiriki katika majadiliano, lakini lazima kuwa na heshima," Maduro amesema katika matamshi yake mapya yaliyorushwa kwenye vyombo vya habari vya serikali ya Venezuela.
"Kwa sasa tuko katika awamu ya kisiasa," amesema Maduro na kusisitiza kuwa, "Lakini ikiwa Venezuela itashambuliwa kwa njia yoyote ile, tutaingia katika hatua ya mapambano ya silaha."
Aliyasema hayo jana Ijumaa, saa chache baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kutishia kuzitungua ndege za kijeshi za Venezuela iwapo 'zitakuwa hatari' kwa majeshi ya Marekani.
Rais Maduro ameeleza bayana kuwa, tofauti kati ya nchi hizo mbili hazitoi uhalali wa kuibuliwa migogoro ya kivita.
Vikosi vya Marekani Jumanne vililipua mashua katika visiwa vya Caribbean, ambayo Trump alidai kuwa ni ya "shirika la uhalifu la Venezuela linalohishwa na Maduro," na kuua watu 11.
Wiki iliyopita, Maduro alisema kuongezeka uwepo wa majeshi ya Marekani katika eneo la Caribbean kunalenga kuipindua serikali yake, na kusisitiza kuwa yuko tayari "kutangaza jamhuri yenye silaha" ikiwa nchi hiyo itashambuliwa na wanajeshi hao wavamizi.
Marekani na Venezuela zimekuwa katika uhasama na misiguano kwa muda mrefu, huku Washington ikiunga mkono viongozi wa upinzani na kuweka vikwazo vinavyolenga kuisakama serikali ya Maduro.