Kansela wa Ujerumani akosoa mashambulizi ya Israel dhidi ya Qatar
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130692-kansela_wa_ujerumani_akosoa_mashambulizi_ya_israel_dhidi_ya_qatar
Friedrich Merz Kansela wa Ujerumani, amekosoa vikali mashambulizi ya utawala wa Israel dhidi ya Doha, Qatar na kutangaza kuwa, Berlin inasubiri matokeo ya mazungumzo na washirika wa Ulaya kuhusu kususia utawala wa Israel.
(last modified 2025-09-12T03:19:07+00:00 )
Sep 12, 2025 03:19 UTC
  • Kansela wa Ujerumani akosoa mashambulizi ya Israel dhidi ya Qatar

Friedrich Merz Kansela wa Ujerumani, amekosoa vikali mashambulizi ya utawala wa Israel dhidi ya Doha, Qatar na kutangaza kuwa, Berlin inasubiri matokeo ya mazungumzo na washirika wa Ulaya kuhusu kususia utawala wa Israel.

Kwa mujibu wa Shirika la Anadolu, Merz amesema katika mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari na Rais wa Baraza la Ulaya Antonio Costa mjini Berlin kwamba mashambulizi ya Israel dhidi ya Doha, Qatar, "yalikiuka sheria za kimataifa, mamlaka ya kitaifa na umoja wa ardhi ya Qatar, ambayo ilikuwa na jukumu la upatanishi katika mgogoro huu (vita vya Gaza) kuliko nchi nyingine yoyote."

Kuhusu pendekezo la Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen la kuwawekea vikwazo mawaziri wenye itikadi kali na walowezi wa Kizayuni na kusimamisha makubaliano ya biashara huria ya Umoja wa Ulaya na Israel, Merz alisema kuwa Berlin na washirika wa Ulaya watalijadili hili katika siku zijazo.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Waziri Mkuu wa Qatar Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al-Thani amelaani mashambulizi ya juzi ya Israel dhidi ya Doha na kuyataja kuwa ni "ugaidi wa kiserikali,". Amesema kuwa Waziri Mkuu wa utawala wa Israel Benjamin Netanyahu anapasa "kufikishwa mbele ya sheria."

Aidha katika taarifa rasmi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar shambulizi hilo lililolenga viongozi wa Hamas limeelezwa kuwa “ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa, likivunja misingi ya mamlaka ya kitaifa na uhuru wa nchi, sambamba na kuhatarisha usalama wa raia.”

Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa mashambulizi hayo ni “ukiukaji wa waziwazi” wa mamlaka ya Qatar, yakifanyika wakati ambapo serikali ya Doha inashiriki kikamilifu katika juhudi za upatanisho wa kusitisha mapigano Gaza na kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas.