Venezuela yatangaza 'maeneo mapya ya ulinzi' mpaka wa Colombia
Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro amesisitiza kujitolea kwa taifa lake kwa amani, uhuru na utu, akizindua mpango mpya wa kuimarisha ulinzi wa ardhi ya nchi hiyo, huku Marekani ikiidhinisha operesheni za CIA katika eneo hilo.
Akihutubia taifa jana Jumatano, Maduro alitangaza kuanzishwa kwa 'Maeneo ya Ulinzi Kamili' katika mpaka wa magharibi wa nchi hiyo na Colombia, yakiwemo majimbo ya Táchira, Apure, na Amazonas, maeneo ambayo kwa muda mrefu yanatazamwa kuwa muhimu kwa usalama wa kitaifa na utulivu wa kikanda.
Maduro amesema, "Sisi ni kielelezo cha utu, ujasiri, na bidii, watu walioazimia kuishi kwa amani na kutetea nchi yetu kwa heshima."
Haya yanajiri baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kuthibitisha jana Jumatano kwamba, ameidhinisha operesheni za Shirika la Ujasusi la Marekani CIA ndani ya ardhi ya Venezuela.
Maduro, ameonya kuwa shambulio lolote dhidi ya taifa lake litakabiliwa kwa mshikamano wa mataifa ya ukanda, akisisitiza kuwa nchi hiyo katu haiwezi kuwa koloni wala kutawaliwa na nguvu za kigeni.
Rais wa Venezuela amesisitiza kuwa: "Hatutawahi kuwa uwanja wa wakoloni, wala watumwa wa dola lolote la kibabe." Amesisitiza kuwa historia ya mapambano ya ukombozi wa bara la Amerika Kusini ni msingi wa mshikamano wa kikanda.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela, Yvan Gil jana Jumatano alishutumu "mienendo ya kijeshi" ya Marekani katika Bahari ya Caribbean, ambayo imepelekea kuuawa takriban raia 27.