Marekani yaitengea Israel dola bilioni 3.3 nyingine za kufanyia jinai duniani
Bunge la Marekani limepasisha muswada wa dola bilioni 3.3 kwa ajili ya utawala wa Kizayuni wa Israel ambao hivi sasa dunia nzima inalaani jinai zake kubwa katika maeneo tofauti hasa huko Palestina na hususan katika Ukanda wa Ghaza.
Televisheni ya Al Alam imetangaza habari hiyo na kunukuu taarifa rasmi ya Marekani ikithibitisha kuwa, chini ya programu wa NSRP ya 2026, Bunge la Marekani limepasisha kupewa Israel kiwango hicho cha fedha kwa jina la msaada wa kijeshi. Wachambuzi wa mambo wanasema, msaada huo ni kama pongezi kwa Israel kutokana na jinai zake za kuchupa mipaka zikiwemo za mashambulizi ya kinyama ya zaidi ya miaka miwili kwenye Ukanda wa Ghaza.
Taarifa ya serikali ya Marekani imesema kuwa, fedha hizo zitasaidia kuhakikisha kwamba mshirika wa Marekani yaani Israel sasa ataweza kukabiliana na vitisho vya kimkakati vya pamoja na kwamba Washington inataka kuwa ina mshirika mwenye nguvu na mwenye uwezo mkubwa katikati ya eneo la Mashariki ya Kati, kama alivyosema.
Israel, utawala unaotenda jinai kubwa zaidi duniani ndiyo inayopokea msaada mkubwa zaidi wa kijeshi kutoka kwa Marekani. Kuna mkataba wa miaka 10 kati ya Marekani na utawala wa Kizayuni ambapo kwa mujibu wa mkataba huo, Israel huwa inapokea takriban dola bilioni 3.3 za silaha zinazofadhiliwa na walipa kodi wa Marekani kila mwaka. Makubaliano hayo yanatarajiwa kumalizika mwaka wa 2028 lakini wachambuzi wa mambo wanasema, mkataba huo lazima utaongezewa muda.
Kwa mujibu wa Chuo Kikuu cha Brown cha Marekani, kufikia Oktoba 7, 2023, Israel ilikuwa imeshapokea msaada wa kijeshi wa dola bilioni 34 kutoka kwa Marekani kupitia makubaliano hayo.