Polisi ya Uturuki yawatawanya walimu kwa mabomu ya kutoa machozi
Polisi ya Uturuki imetumia mabomu ya kutoa machozi kutawanya mamia ya walimu waliofanya maandamano kulalamikia hatua ya serikali ya kuwapiga kalamu nyekundu walimu wenzao kwa sababu za kisiasa katika mji wa Diyarbakır.
Vyombo vya habari nchini Uturuki vimeripoti kwamba, mamia ya walimu jana Jumamosi walimiminika mabarabarani katika mji huo kupinga hatua ya kusimamishwa kazi zaidi ya walimu elfu 10 kwa tuhuma za kushirikiana na chama cha PKK ambapo walipiga kambi mbele ya idara ya Elimu na Mafunzo ya Diyarbakır. Katika maandamano hayo walimu walipiga nara dhidi ya ukandamizaji wa serikali dhidi ya walimu na kusema kuwa mwenendo huo haupasi kufumbiwa macho. Hata hivyo polisi iliyataja maandamano hayo kuwa yasiyo halali ambapo kabla ya kuwashambulia walimu hao, iliwataka kutawanyika mara moja. Kutokana na waandamanaji kutotii amri ya polisi walishambuliwa kwa mabomu ya kutoa machozi na kutawanywa. Kwa akali walimu 30 walitiwa mbaroni katika maandamano hayo.
Alkhamis iliyopita, serikali ya Uturuki kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya nchi hiyo ilitangaza kuwasimamisha kazi walimu elfu 11 na 500. Serikali inawatuhumu watu hao kwa kuunga mkono chama cha PKK. Afisa mmoja wa serikali ya Ankara amenukuliwa akisema kuwa, walimu hao wataendelea kuwa nje ya kazi hadi utakapomalizika uchunguzi dhidi yao. Inafaa kuashiria kuwa, tangu kulipojiri mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli, serikali ya Uturuki imekuwa ikiwafuta na kuwasimamisha kazi wafanyakazi wa taasisi mbalimbali za kiraia na serikali.