Rais Rouhani: NAM inaweza kutatua matatizo ya dunia
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa wito wa kuwepo ushirikiano zaidi baina ya nchi wananchama wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM.
Akizungumza katika mkutano wa 17 wa NAM katika Kisiwa cha Margarita nchini Venezuela, Jumamosi, Rais Rouhani amesema hivi sasa, zaidi ya wakati wowote ule, wanachama wa NAM wanahitaji mshikamano na ushirikiano. Amesema NAM ni kundi ambalo wanachama wake ni karibu robo tatu ya wanachama wote wa Umoja wa Mataifa na kwa hivyo nchi hizo zina nafasi isiyopingika katika kutatua matatizo ya leo duniani.
Amesema kufungamana na misingi ya NAM ni jambo litakalodhamini uhuru, ulinzi wa mipaka na mamlaka ya kujitawala nchi zote sambaba na kuimarisha maslahi ya kitaifa, ujirani mwema, usalama na ustawi endelevu kote duniani.
Rouhani amesema kukiukwa mamlaka ya kujitawala nchi tofauti duniani ni tishio kwa usalama wa dunia. Akigusia migogoro iliyoibuliwa katika Mashariki ya Kati na Afrika katika miaka ya hivi karibuni, Rais Rouhani amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa nchi ya kwanza kuonya kuhusu tishio la ugaidi wa kitafkiri nchini Syria. Ameongeza kuwa, wakati baadhi ya nchi zisizowajibika Mashariki ya Kati na Magharibi zilipokuwa zikiwapa silaha magaidi wa kitakfiri, taifa la Iran lilisimama pamoja na mataifa ya Syria na Iraq katika vita dhidi ya makundi hatari zaidi ya kigaidi.
Rais wa Iran amesema nchi ambazo zinaunga mkono magaidi wa Kitafkiri zilianzisha muugano eti wa kupambana na magaidi lakini kile kinachoshuhudiwa sasa ni kuongezeka magaidi duniani. Rais Rouhani katika hotuba yake pia ameashiria kadhia ya Palestina na kusema utawala wa Kizyauni unatumia vibaya matukio ya Mashariki ya kati hasa kuibuka makundi ya kigaidi kama ISIS ili kufunika jinai zake dhidi ya taifa linalodhulumiwa la Palestina.
Mwishoni mwa kikao hicho, Rais Rouhani alimkabidhi rasmi mwenzake wa Venezuela Nicolas Maduro uenyekiti wa mzunguko wa NAM. Mkutano huo umewaleta pamoja marais na wajumbe wa nchi 120 wanachama.