Cyprus yakubali kumrejesha Misri mtekaji nyara wa ndege ya EgyptAir
(last modified Sat, 01 Oct 2016 04:22:18 GMT )
Oct 01, 2016 04:22 UTC
  • Cyprus yakubali kumrejesha Misri mtekaji nyara wa ndege ya EgyptAir

Mahakam moja nchini Cyprus imetoa hukumu ya kurejeshwa Misri raia mmoja wa nchi hiyo aliyeiteka nyara ndege ya shirika la EgyptAir mwanzoni mwa mwaka huu.

Mtandao wa habari wa Daily News wa nchini Misri umeripoti habari hiyo na kusema kuwa, jana (Ijumaa) jaji wa mahakama hiyo Donna Costantino alikubali ombi la serikali ya Misri la kumrejea nchini humo Seif El-Din Mustafa aliyeiteka nyara ndege ya EgyptAir ilikuwa katika safari za ndani ya Misri na kuipelekea nchini Cyprus.

Shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa, Seif El-Din Mustafa atakabidhiwa kwa serikali ya Misri katika kipindi cha siku kumi zijazo na hadi wakati huo atakuwa mikononi mwa polisi wa Cyprus. 

Raia huyo wa Misri alisema kuwa, shabaha yake ilikuwa ni kuwafanya walimwengu wajue mateso wanayopata wananchi wa Misri kutoka kwa serikali inayoungwa mkono na jeshi la nchi hiyo, na kamwe hakuwa na nia ya kumdhuru mtu yeyote yule. 

Nege ya Misri iliyotekwa nyara Machi 29, 2016 na raia wa Misri Seif El-Din Mustafa na kupelekwa Cyprus. Hapa wanaoneka abiria wa mwisho wakitoka kwenye ndege hiyo kupitia dirishani.

 

Vile vile alisema mahakami kuwa, lengo lake jingine lilikuwa ni kuilazimisha serikali ya Rais Abdul Fattah el Sisi iwaachilie huru wasichana 63 wanafunzi wa vyuo vikuu vya Misri ambao wako jela.

Seif El-Din Mustafa alijitahidi sana kuizuia mahakama ya Cyprus isimkabidhi kwa serikali ya Misri na kusema kuwa, hatua hiyo itakuwa ni kupiga muhuri wa mateso na kifo chake mikononi mwa maafisa wa Misri. 

Wakili wa mtuhumiwa huyo amesema, mteja wake amemtaka apinge hukumu hiyo na asiruhusu akabidhiwe kwa maafisa wa serikali ya Misri. 

Utekaji nyara huo ulimalizika tarehe 29 Machi mwaka huu nchini Cyprus baada ya kuachiliwa huru watu wote 72 waliokuwemo kwenye ndege hiyo wakiwemo wahudumu, na baadaye kutiwa mbaroni mtekaji nyara huyo.