Mamilioni ya Waislamu wakumbuka tukio la kuuawa shahidi Imam Hussein (as)
Mamilioni ya Waislamu wa madhehebu ya Shia leo tarehe 9 Muharram wameshirika katika shughuli ya kukumbuka tukio chungu la kuuawa mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw), Imam Hussein (as).
Hapa nchini Iran shughuli za kukumbuka mauaji ya Imam Hussein (as) zimeshuhudiwa katika miji mbalimbali hususan katika miji mitakatifu ya Mash'had na Qum ambapo mamilioni ya watu walikusanyika misikitini, katika kumbi za kidini na maeneo mengine ya ibada na ya kijamii kukumbuka tukio chungu la kuuawa shahidi Imam Hussein bin Ali (as).
Majlisi na vikao vya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume wetu Muhamamd (saw), Imam Hussein (as) zimefanyika pia katika nchi mbalimbali ambapo Waislamu hususan wafuasi wa na wapenzi wa Watu wa Nyumba ya Mtume wetu Muhammad (saw) wamekusanyika na kukumbuka tukio hilo chungu.
Kilele cha shughuli za kukumbuka tukio chungu la kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume kitakuwa kesho tarehe 10 Muharram ambayo ni maarufu kwa jila la Ashuraa.
Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) aliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 baada ya kuamua kupambana na mtawala dhalimu na muovu wa kizazi cha Bani Umayyah Yazid bin Muawiya aliyebadili mafundisho ya dini.