Umoja wa Mataifa wakosoa mienendo hasi ya utawala haramu wa Israel
Michael Lynk, Mwakilisi Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Haki za Binaadamu katika ardhi za Palestina, amesema kuwa Israel inazuia shughuli za makundi ya kutetea haki za binaadamu.
Sanjari na kubainisha suala hilo, Lynk amesema kuwa kuna udharura wa kuchunguzwa vitendo vya ukiukaji wa haki za binaadamu vinavyofanywa na Tel Aviv. Kadhalika ametangaza kuwa, mienendo hiyo hasi ya utawala wa Kizayuni juu ya ukandamizaji wa haki za binaadamu eneo la Mashariki ya Kati, itachunguzwa karika ripoti itakayofuatia ya umoja huo.
Katika miaka ya hivi karibuni kumetolewa ripoti kadhaa zilizo kinyume na ubinaadamu na ukatili vinavyotekelezwa na utawala huo khabithi dhidi ya makundi ya watetezi wa haki za binaadamu huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa juu ya miamala mibaya ya Israel, imetolewa katika hali ambayo hadi sasa umoja huo haujatoa radiamali yoyote ya maana juu ya udhalilishaji unaofanywa na maafisa wa utawala huo dhidi ya wawakilishi wa jamuiya za kimataifa katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha miamala isiyofaa ya Tel Aviv dhidi ya makundi hayo ya wanaharakati wa haki za binaadamu na kamisheni za kufuatilia uhakika za Umoja wa Mataifa, inabainisha wazi kwamba suala la haki za binaadamu, halina nafasi katika siasa za utawala huo pandikizi.
Vyombo vya sheria vinariopoti kuzuiwa maripota maalumu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa kwenda ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo wa Kizayuni. Hakuna shaka kwamba miamala hiyo ndiyo imezifanya asasi mbalimbali kuutaja utawala huo kuwa wa kibaguzi. Mnafaa kufahamu kwamba, katika kuamiliana vibaya na wanaharakati wa kimataifa, Israel haiheshimu mpaka wowote katika fremu hiyo, na Tel Aviv ina historia mbaya ya vitendo hivyo kukiwemo kushambulia meli zilizobeba wanaharakati wa amani na misaada ya kibinaadamu kwa ajili ya raia madhlum wa Palestina. Mwaka 2010 askari wa Israel, walishambulia msafara wa baharini uliopewa jina la 'Uhuru wa Gaza' na ambao ulizijumuisha meli sita zilizokuwa zimebeba wanaharakati wa amani 663 kutoka nchi 37 za dunia.
Hujuma hiyo ilitekelezwa wakati ambao meli hizo zilikuwa katika maji ya kimataifa ambapo wanaharakati tisa waliuawa na wengine 60 kujeruhiwa. Hivi karibuni pia kitendo cha utawala huo katili cha kuwaondoa wanaharakati wa haki za binaadamu ambao walikuwa wanakusudia kuelekea Ukanda wa Gaza kwa lengo la kuvunja mzingiro dhidi ya eneo hilo, kimebainisha ukweli huu kwamba, Israel haiheshimu hata kidogo haki za wanaharakati wa amani.
Hii ni katika hali ambayo hivi karibuni pia, Israel na kwa jeuri kabisa ilitangaza kuwaondoa abiria wote waliokuwa ndani ya meli ya misaada iliyopewa jina la 'Mashua ya Wanawake Kuelekea Gaza' hatua ambayo ilitekelezwa baada ya kuizuia meli hiyo kuingia ukanda huo ambao umekuwa chini ya mzingiro wa kila upande kwa kipindi cha miaka kadhaa sasa. Jumla ya wanawake 13 akiwemo Mairead Maguire, mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel kutoka Ireland Kaskazini, walitiwa mbaroni na askari wa utawala huo baada ya meli yao kusimamishwa karibu na maili 35 za pwani ya Gaza na kisha kuondoshwa eneo hilo.
Mienendo hiyo ya kila uchao ya kifedhuli inayotekelezwa na Israel dhidi ya wanaharakati wa kimataifa, ndiyo imeufanya mara hii Umoja wa Mataifa kuweza kutoa sauti ya malalamiko yake. Inaelezwa kuwa, kutokana na wasi wasi ilionao wa kufichuka jinai zake mbele ya taasisi za kimataifa, hatua ambayo itatoa mwanya wa kuchunguzwa jinai hizo, Israel inafanya kila iwezalo kuzuia wanaharakati kuweza kufika ardhi za Palestina ili kujionea uhalisia wa mambo juu ya ukatili wa kutisha wa Tel Aviv. Ukubwa wa jinai za utawala huo, umepelekea kuwa wazi kiasi cha kumfanya kila mtu au asasi za kimataifa kuanza uchunguzi, suala ambalo limeufanya uweze kuchukiwa kila pembe ya dunia.
Hakuna shaka kuwa, kulegalega misimamo ya jumuiya za kimataifa katika kufuatilia mienendo hasi ya Israel dhidi ya wanaharakati wa haki za binaadamu na kadhalika uungaji mkono wa kila upande wa madola ya Magharibi kwa Tel Aviv, vimekuwa na nafasi muhimu katika kuuchochea utawala huo pandikizi kuweza kuendeleza jinai na mienendo yake hiyo kila uchao.