Italia yakanusha tuhuma za kuwatesa wahajiri wa Kiafrika
Polisi ya Italia imepinga ripoti iliyotolewa na shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International kwamba, askari usalama wa nchi hiyo walitumia mabavu na mateso dhidi ya wakimbizi wa Kiafrika.
Mkuu wa Polisi ya Italia, Franco Gabrielli amesema kuwa anapinga ripoti hiyo ya Amnesty International kwamba polisi wa nchi hiyo wanatumia mabavu na kuwatesa wakimbizi. Shirika hilo la haki za binadamu lilisema jana kuwa, polisi wa Italia wamekuwa wakiamiliana na wahajiri kwa namna ambayo inahesabiwa kuwa ni mateso wakati wa kuchukua alama za vidole ili kuingia nchini humo.
Tuhuma hizo za kuwatesa wakimbizi ni pamoja na kuwapiga, kuwatesa kwa kutumia umeme na udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wakimbizi wa Kiafrika wanaotafuta hifadhi katika nchi nyingine za Ulaya kupitia Italia.
Baada ya kufungwa njia zote za nchi kavu, njia ya majini kupitia Bahari ya Mediterania kuelekea Italia imesalia kuwa njia kuu kwa wahajiri wanaotafuta hifadhi barani Ulaya wakikimbia mapigano katika nchi za Kiafrika.