UN yakosoa kuendelea ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i20086-un_yakosoa_kuendelea_ujenzi_wa_vitongoji_vya_walowezi_wa_kiyahudi
Umoja wa Mataifa umelaani uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kujenga nyumba 500 mpya mashariki mwa Baitul Muqaddas.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Nov 24, 2016 04:34 UTC
  • UN yakosoa kuendelea ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi

Umoja wa Mataifa umelaani uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kujenga nyumba 500 mpya mashariki mwa Baitul Muqaddas.

Nikolay Mladenov Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Mashariki ya Kati amelaani uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa kujenga nyumba mpya za walowezi wa Kiyahudi huko katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan khususan mashariki mwa Baitul Muqaddas; na kuutaka utawala huo kusitisha hatua zake hizo zilizo kinyume cha sheria.

Nikolay Mladenov Mjumbe Maalumu wa UN katika Mashariki ya Kati

Mladenov amesema akiwa katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa matukio ya hivi karibuni huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu yanatia wasiwasi mkubwa. Nikolay Mladenov amebainisha kuwa, viongozi wa Israel wametakiwa wazingatie maombi ya mara kwa mara yanayotolewa ili utawala huo usimamishe ujenzi ulio kinyume cha sheria wa nyumba za walowezi wa Kiyahudi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan; ukiwemo ujenzi unaofanywa na Israel huko Baitul Muqaddas mashariki. 

Baadhi ya nyumba za walowezi wa Kiyahudi zilizojengwa huko Baitul Muqaddas ya mashariki

Ripoti iliyotolewa na shirika moja lisilo la kiserikali imeeleza kuwa, Israel jana ilianza tena miradi yake ya kujenga nyumba mpya 500 za walowezi wa Kiyahudi huko Baitul Muqaddas ikiwa ni hatua yake ya kwanza  baada ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa Rais wa Marekani hivi karibuni. Israel ililivamia na kulikalia kwa mabavu eneo la Baitul Muqaddas ya mashariki mwaka 1967 ambayo ni ardhi ya Palestina; hatua ambayo imepingwa na kulaaniwa na jamii ya kimataifa.