Wamarekani milioni 4.7 wawataka wajumbe wa majimbo watengue kura walizompa Trump
https://parstoday.ir/sw/news/world-i20632-wamarekani_milioni_4.7_wawataka_wajumbe_wa_majimbo_watengue_kura_walizompa_trump
Wamarekani wapatao milioni nne na laki saba wamesaini kupitia mtandao wa intaneti ujumbe wa ombi kwa wajumbe wa majimbo (Electoral College) la kuwataka watengue kura walizompigia rais mteule wa nchi hiyo Donald Trump na kumuunga mkono mgombea aliyeshindwa wa chama cha Democrat, Hillary Clinton.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 03, 2016 04:24 UTC
  • Wamarekani milioni 4.7 wawataka wajumbe wa majimbo watengue kura walizompa Trump

Wamarekani wapatao milioni nne na laki saba wamesaini kupitia mtandao wa intaneti ujumbe wa ombi kwa wajumbe wa majimbo (Electoral College) la kuwataka watengue kura walizompigia rais mteule wa nchi hiyo Donald Trump na kumuunga mkono mgombea aliyeshindwa wa chama cha Democrat, Hillary Clinton.

Barua hiyo ya ombi ilitayarishwa mwezi uliopita wa Novemba na Daniel Brezenoff, mwanaharakati wa kijamii na lengo lake ni kuweza kukusanya saini zisizopungua milioni sita za Wamarekani wanaopinga ushindi wa Trump aliopata kupitia kura za wajumbe wa majimbo katika uchaguzi wa rais wa Marekani uliofanyika tarehe 8 ya mwezi uliopita wa Novemba.

Brezenoff ametoa hoja katika barua hiyo ya malalamiko kwamba kwa kuwa Hillary Clinton amepata kura nyingi zaidi za wananchi, wajumbe wa majimbo wanapaswa kuheshimu matakwa ya wananchi.

Barua hiyo ya ombi imeeleza kuwa, kwa mtazamo wa kisheria wajumbe wa majimbo wanaweza kubadilisha uamuzi wao katika kura walizopiga; hivyo ifikapo tarehe 19 Desemba ambapo wataidhinisha rasmi kura zao hizo kwa rais, wampigie kura Hillary Clinton kwa kufuata matakwa ya wananchi waliowengi.

Wamarekani waandamana kupinga mfumo wa kura za wajumbe wa majimbo

Ikumbukwe kuwa Donald Trump aliibuka mshindi katika uchaguzi wa rais wa Marekani baada ya kushinda kura za wajumbe wa majimbo zaidi ya 270 yanayohitajika kumwezesha mgombea kushinda uchaguzi huo.

Trump alishinda majimbo 306 kati ya majimbo yote 538 na kumwacha nyuma Clinton aliyeambulia majimbo 232.

Hata hivyo katika kura za wananchi Bi Hillary Clinton alishinda kwa kujipatia kura milioni 64 kulinganisha na milioni 62 alizopata Donald Trump.../