Mbunge Mwislamu adhalilishwa na dereva wa teksi Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i21001-mbunge_mwislamu_adhalilishwa_na_dereva_wa_teksi_marekani
Mbunge wa kwanza mwenye asili ya Kisomali kuchaguliwa nchini Marekani amesema dereva mmoja wa teksi amemdhalilisha na kumtolea maneno ya chuki dhidi ya Uislamu mjini Washington.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Dec 08, 2016 04:06 UTC
  • Mbunge Mwislamu adhalilishwa na dereva wa teksi Marekani

Mbunge wa kwanza mwenye asili ya Kisomali kuchaguliwa nchini Marekani amesema dereva mmoja wa teksi amemdhalilisha na kumtolea maneno ya chuki dhidi ya Uislamu mjini Washington.

Ilhan Omar, ambaye aliwahi kuwa mkimbizi nchini Marekani na ambaye alichaguliwa kuwa mbunge wa Minnesota katika uchaguzi uliofanyika mwezi uliopita, amechapisha kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook kuwa: "Nilipokuwa nikiondoka kwenye mkutano wa sera katika Ikulu ya White House nikielekea hotelini, nilikumbana na tukio la kibaguzi na chuki ambalo sijawahi kulishuhudia tena. Dereva wangu wa teksi alianza kunitolea maneno ya chuki na kuniita mfuasi wa kundi la kigaidi la ISIS huku akitishia kunivua hijabu."

Mtunga sheria huyo wa Kisomali ameongeza kuwa: "Sielewi watu wanatoa wapi ujasiri wa kueneza wazi wazi chuki zao dhidi ya Waislamu."

Chuki dhidi ya Uislamu nchini Marekani zimeongezeka mno tangu kuchaguliwa Trump

Haya yanajiri katika hali ambayo, gazeti la New York Times linalochapishwa nchini Marekani liliashiria katika ripoti yake ya hivi karibuni kuwa, uhalifu unaotokana na chuki na vitendo vya ubaguzi wa rangi kote nchini Marekani umeongezeka mno tangu kuchaguliwa Donald Trump  kuwa rais mpya wa nchi hiyo.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, mwishoni mwa mwezi uliopita wa Novemba, Masjidul Karim wa mji wa Providence huko Rhode Island nchini Marekani ulitumiwa barua yenye chuki za kidini dhidi ya Waislamu. Miongoni mwa maneno yaliyokuwemo kwenye barua hiyo yanasema: 'Donald Trump, rais mteule wa Marekani atawatendea maovu Waislamu kuliko vile Hitler alivyowatendea Mayahudi.'