Ban akariri wito wa kuwekewa vikwazo vya silaha Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/world-i21778-ban_akariri_wito_wa_kuwekewa_vikwazo_vya_silaha_sudan_kusini
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuwa Sudan Kusini iko katika ncha ya kushuhudia mauaji ya kimbari iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa, huku akikariri wito wake wa kutaka nchi hiyo iwekewe vikwazo vya silaha.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 20, 2016 04:28 UTC
  • Ban akariri wito wa kuwekewa vikwazo vya silaha Sudan Kusini

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuwa Sudan Kusini iko katika ncha ya kushuhudia mauaji ya kimbari iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa, huku akikariri wito wake wa kutaka nchi hiyo iwekewe vikwazo vya silaha.

Akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana Jumatatu, Ban Ki-moon ambaye siku chache zijazo muda wake wa kuhudumu utamalizika alisema: "Iwapo tutafeli kufanya maamuzi magumu, Sudan Kusini itatumbukia katika mauaji ya kikabila na ya umati. Baraza la Usalama lazima lichukue hatua kuhakikisha kuwa mizizi ya mzunguko wa silaha nchini humo inakatwa."

Ban Ki-moon, Katibu Mkuu anayeondoka wa Umoja wa Mataifa

Kauli ya Ban inajiri siku chache baada ya Mjumbe wa Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini kusema kuwa, kumetokea mauaji ya kimbari katika maeneo kadhaa ya Sudan Kusini.

Yasmin Sooka aliyasema hayo mapema mwezi huu mjini Geneva Uswisi baada ya kurejea kutoka safari ya siku 10 ya kuitembelea Sudan Kusini na kufafanua kwamba, mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini humo yanafanana na yale yaliyotokea mwaka 1994 nchini Rwanda. Amesema, mauaji ya kimbari Sudan Kusini yametokea kwa mfululizo na kuna uwezekano hali ya nchi hiyo ikawa sawa na ile ya Rwanda mwaka 1994.

Hata hivyo, Akuei Bona Malwal, Balozi wa Sudan Kusini katika Umoja wa Mataifa ameyakanusha madai hayo na kusisitiza kuwa, hali sio mbaya kiasi hicho, kama inavyotaka kuonyesha UN.

Rais Salva Kiir na makamu wake wa zamani Riek Machar

Tangu mwezi Disemba 2013 wakati ulipoanza mgogoro baina ya Rais Salva Kiir na makamu wake wa zamani Riek Machar, raia milioni tatu wa Sudan Kusini wamekuwa wakimbizi mbali na mauaji ya makumi ya watu.