Mayahudi wa Othodoksi waunga mkono azimio la UN dhidi ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i22408-mayahudi_wa_othodoksi_waunga_mkono_azimio_la_un_dhidi_ya_israel
Idadi kadhaa ya Mayahudi wa madhehebu ya Othodoksi wamekusanyika mbele ya Ikulu ya Rais wa Marekani, White House kuonyesha uungaji mkono wao kwa azimio lililopitishwa karibuni na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kulaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na utawala haramu wa Israel katika ardhi unazozikalia kwa mabavu za Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 30, 2016 03:36 UTC
  • Mayahudi wa Othodoksi waunga mkono azimio la UN dhidi ya Israel

Idadi kadhaa ya Mayahudi wa madhehebu ya Othodoksi wamekusanyika mbele ya Ikulu ya Rais wa Marekani, White House kuonyesha uungaji mkono wao kwa azimio lililopitishwa karibuni na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kulaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na utawala haramu wa Israel katika ardhi unazozikalia kwa mabavu za Palestina.

Waandamanaji hao wametaka kufutiliwa mbali haraka dola bandia la Israel na kurejeshewa Wapalestina ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu.

Kiongozi wa Mayahudi hao waliokusanyika mbele ya White House amesema: "Tukiwa ni Mayahudi, tunasononeka na kuona aibu kwa kuwa jinai hizi zote zinafanywa kwa jina letu". Aidha amesema: "Huku ni kuvunjia heshima dini yetu; inasikitisha kwamba dini yetu inatumiwa vibaya ili kuhalalisha jinai zote hizi".

Kiongozi wa madhehebu ya Kiyahudi ya Othodoksi ameendelea kueleza kwamba "Tuna matumaini kuwa azimio lililopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litawezesha kuhitimishwa utumiaji mbaya wa jina langu, jina la watu wangu na jina la Mayahudi".

Kiongozi wa Mayahudi akizungumza mbele ya White House

Waandamanaji hao aidha wameeleza kuchukizwa kwao na uungaji mkono wa fedha na silaha wa Marekani kwa utawala haramu wa Israel na kutaka kukomeshwa jinai za utawala huo ghasibu dhidi ya Wapalestina.

Itakumbukwa kuwa siku ya Ijumaa iliyopita, katika hatua isiyo ya kawaida, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio la kulaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi zilizoghusubiwa za Palestina. Azimio hilo nambari 2334 limeutaka utawala wa Kizayuni usimamishe haraka na kikamilifu shughuli za ujenzi wa vitongoji katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu ikiwemo Baitul Muqaddas Mashariki…/