Jan 19, 2017 14:25 UTC
  • Pakistan yapinga kuhamishwa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv kwenda Quds

Mwakilishi wa Kudumu wa Pakistan katika Umoja wa Mataifa amepinga hatua yoyote ya uhamishaji wa ubalozi wa Marekani kutoka Tel-Aviv, Israel kwenda Baytul-Muqaddas na kwamba, kitendo hicho ni ukiukaji wa wazi wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Maleeha Lodhi, ameyasema hayo katika kupinga matamshi ya rais mteule wa Marekani Donald Trump, ya kutaka kuhamishiwa ubalozi wa nchi hiyo kutoka mji mkuu wa utawala wa Kizayuni Tel Aviv kwenda Quds Tukufu na kuongeza kuwa, kupatikana taifa huru la Palestina kunadhaminiwa na mji mkuu wake kuwa Baytul-Muqaddas na si vinginevyo.

Ubalozi wa Marekani uliopo Tel Aviv unaokusudiwa kuhamishiwa Quds

Lodhi amesema kuwa, kwa zaidi ya nusu karne sasa, utawala wa Kizayuni ambao kwa kutoheshimu maazimio na sheria za Umoja wa Mataifa, umeendelea kuyakalia kwa mabavu maeneo ya Ukingo wa Mto Jordan sambamba na kuyafanya maisha ya raia asili wa Palestina kuwa magumu zaidi. Mwakilishi huyo wa Kudumu wa Pakistan katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, Baytul-Muqaddas ni moyo wa ulimwengu wa Kiislamu na kwamba, tukio lolote linalotokea Palestina na wakazi wake, litakuwa na taathira kwa eneo zima la Mashariki ya Kati na dunia kwa ujumla.

Baytul-Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu hadi sasa na utawala haramu wa Kizayuni

Katika kampeni zake za urais, Donald Trump aliashiria kuwa kama angechaguliwa kuwa rais wa Marekani angetekeleza mpango huo, suala ambalo lilikabiliwa na radiamali nyingi kali kieneo na kimataifa.

Tags