Mexico wasusia bidhaa za Marekani, wamlaani Donald Trump
https://parstoday.ir/sw/news/world-i24569-mexico_wasusia_bidhaa_za_marekani_wamlaani_donald_trump
Wananchi wa Mexico wameamua kuonesha hasira zao kupitia kususia bidhaa za Marekani ikiwa ni kulalamikia matamshi ya hivi karibuni ya Donald Trump, rais wa nchi hiyo ya kibeberu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 01, 2017 23:21 UTC
  • Mexico wasusia bidhaa za Marekani, wamlaani Donald Trump

Wananchi wa Mexico wameamua kuonesha hasira zao kupitia kususia bidhaa za Marekani ikiwa ni kulalamikia matamshi ya hivi karibuni ya Donald Trump, rais wa nchi hiyo ya kibeberu.

Mtandao wa lugha ya Kifarsi wa Televisheni ya Press TV umetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, wananchi hao wanaendesha kampeni maalumu katika mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter na Instagram chini ya kaulimbiu: "Sisi sote ni Wamexico" na kuandika maneno mbalimbali ya kumlaani Trump na kuonesha msimamo wa kuihami nchi yao mbele ya siasa za kijuba za rais mpya wa Marekani.

Wananchi hao wa Mexico wameanzisha kampeni maalumu pia ya kususia bidhaa za Marekani na wamefanya maandamano mbele ya ubalozi wa nchi huko Mexico City, mji mkuu wa Mexico kulaani hatua ya Donald Trump ya kuamua kujenga ukuta kwenye mpaka wa nchi hizo mbili ili kuzuia wakimbizi kuingia Marekani. Mexico inapakana na Marekani upande wake wa kusini.

Waandamanaji walioandamana nje ya ubalozi wa Marekani mjini Mexico City wakiwa wamechoma moto kinyago chenye pembe za bendera ya Marekani

 

Msemaji wa Rais wa Mexico pamoja na mawaziri wa Mambo ya Nje na Fedha wa nchi hiyo wameamua kuweka picha za bendera ya Mexico katika profile za kurasa zao za Twitter. 

Mashirika ya Marekani yanamimina bidhaa nyingi kwenye soko la Mexico, na iwapo wananchi wa nchi hiyo wataamua kikweli kweli kususia bidhaa za Marekani, mashirika ya nchi hiyo ya kibeberu yatapata hasara kubwa.

Kwa upande wake, Rais Enrique Peña Nieto wa Mexico amewashukuru wananchi wa nchi hiyo kwa kuonesha mshikamano na mapenzi makubwa kwa nchi yao na kusema kuwa, hatua hiyo inapaswa kuwa jiwe la msingi la hatua za kiistratijia za ndani na nje ya Mexico.