Kuendelea maandamano ya Wamexico dhidi ya pendekezo la Trump
https://parstoday.ir/sw/news/world-i25340-kuendelea_maandamano_ya_wamexico_dhidi_ya_pendekezo_la_trump
Maelfu ya raia wa Mexico wamefanya maandamano makubwa katika kulalamikia mpango wa ujenzi wa ukuta wa Rais Donald Trump wa Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 19, 2017 03:01 UTC
  • Kuendelea maandamano ya Wamexico dhidi ya pendekezo la Trump

Maelfu ya raia wa Mexico wamefanya maandamano makubwa katika kulalamikia mpango wa ujenzi wa ukuta wa Rais Donald Trump wa Marekani.

Wamexico wamefanya maandamano hayo katika mpaka wa nchi hiyo na Marekani ambapo wameunda mfano wa ukuta wa binaadamu na kulalamikia hatua ya rais huyo mpya wa Marekani ya kutaka kuzitenga nchi mbili hizo kwa ukuta. Kadhalika waandamanaji wamelitaja pendekezo hilo la Rais Trump kuwa ni ubaguzi na uadui wa wazi dhidi ya nchi yao. Hii sio mara ya kwanza kwa raia wa Mexico kufanya maandamano ya kulalamikia siasa mbovu za uhajiri zinazotekelezwa na serikali mpya ya Washington.

Wamexico wakiwa katika maandamano

Hivi karibuni maelfu ya wananchi wa Mexico walifanya maandamano makubwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Mexico City wakitaka kuheshimiwa nchi yao pamoja na wahajiri wa nchi hiyo. Maandamano hayo yalifanyika kufuatia matamshi ya chuki na uhasama ya Trump na serikali yake dhidi ya wahajiri na Wamexico. Wimbi la maandamano lilianza mwezi uliopita pale Rais Trump alipotia saini amri ya kuruhusu ujenzi wa ukuta katika mpaka wa nchi mbili na kutaka kuharakishwa kuondolewa wahajiri haramu kutoka Marekani.

Sehemu nyingine ya maandamano ya Wamexico dhidi ya Trump

Aidha katika harakati nyingine iliyoibua makelele na tofauti kubwa kati ya mataifa hayo ni hatua ya Trump kumtaka Rais Enrique Peña Nieto wa Mexico kulipa gharama za ujenzi wa ukuta huo wa mpakani. Hii  ni katika hali ambayo kwa mara kadhaa Rais Peña Nieto amekuwa akisisitiza kuwa kamwe nchi yake haitolipa gharama za ujenzi wa ukuta huo. Katika kupinga ombi hilo la Rais Donald Trump, rais wa Mexico alivunja safari yake kuelekea Washington kwa ajili ya kukutana na rais huyo wa Marekani. Kwa upande wake serikali ya Trump imeendelea kusisitizia ujenzi wa ukuta huo katika mpaka wa nchi hizo mbili.

Rais Enrique Peña Nieto wa Mexico akiwa na Trump siku za nyuma

Katika hilo White House imetangaza kuwa, rais wa nchi hiyo amekusudia kulipa gharama za ujenzi wa ukuta uliotajwa wenye urefu wa kilometa 3200 kupitia ongezeko la asilimia 20 ya kodi inayotozwa bidhaa zinazotoka Mexico kuingia Marekani. Hata hivyo muda punde baada ya pendekezo hilo, kuliibuka wimbi la ukosoaji dhidi ya ongezeko hilo la kodi kati ya wanasheria wa Marekani. Wanaharakati wa haki za binaadamu nchini Marekani wameutaja mpango wa ujenzi wa ukuta huo kuwa ni sawa na ukandamizaji wa uhuru wa raia na katika hilo wanaamini kuwa ujenzi huo utaibua utengano wa kibinadamu na kiutamaduni kati ya raia wa Marekani na Mexico. Hata hivyo siasa za kiuhasama za Trump hazijaishia kwenye ujenzi wa ukuta huo.

Hivi karibuni rais huyo alitoa amri ya kuzuia raia wa nchi saba za Kiislamu kuingia Marekani kwa madai ya kulinda usalama wa nchi yake. Amri hiyo isiyo kuwa na mantiki mbali na kupingwa na raia wa Marekani, ilipingwa vikali pia na majaji wa nchi hiyo. Majaji walisisitiza kuwa raia wa mataifa hayo saba ya Kiislamu hawajahusika kwa aina yoyote na vitendo vya ugaidi nchini Marekani na hivyo kuamuru kutotekelezwa marufuku ya rais huyo. Ukweli ni kwamba siasa za kibaguzi za Donald Trump ambazo ziko dhidi ya ubinaadau, zimeibua chuki katika jamii sambamba na kupatikana ombwe la mahusiano baina ya Marekani na nchi nyingine za dunia na ni kwa msingi huo ndio maana kukaendelea kushuhudiwa maandamano dhidi ya rais huyo hata nje ya mipaka ya Marekani. Hatua ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Mexico ya kuwataka raia wake walioko nchini Marekani kuwa waangalifu, inadhihirisha kuwa hivi sasa Marekani sio tena mahala salama kwa raia, wafanyakazi, wanafunzi na watu wenye vipawa vya elimu wa nchi nyingine.