Mwito wa UN wa kuwekewa vikwazo utawala wa Kizayuni wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i26112-mwito_wa_un_wa_kuwekewa_vikwazo_utawala_wa_kizayuni_wa_israel
Kamishna Mkuu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ametoa muswada mpya wa kuzitaka nchi za dunia kuacha kufanya biashara yoyote ile na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 09, 2017 00:36 UTC
  • Mwito wa UN wa kuwekewa vikwazo utawala wa Kizayuni wa Israel

Kamishna Mkuu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ametoa muswada mpya wa kuzitaka nchi za dunia kuacha kufanya biashara yoyote ile na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.

Katika muswada wake huo, Zeid bin Ra'ad Zeid al-Hussein ameushutumu utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa unapora ardhi za Wapalestina na kujenga vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni, hivyo nchi zote duniani zinapaswa kususia kitu chochote kinachotoka kwenye vitongoji hivyo.

Kabla ya hapo pia, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikuwa limepasisha azimio tarehe 23 Disemba 2016 na sambamba na kulaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi wanazoporwa Wapalestina, liliutaka utawala wa Kizayuni kusimamisha mara moja ujenzi wa vitongoji hivyo.

Zeid bin Ra'ad Zeid al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

 

Hasira za walimwengu na jamii ya kimataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni ni kubwa sana, na kila leo zinaongezeka kutokana na Israel kuendelea kuwakandamiza wananchi madhulumu wa Palestina na kuwapora haki zao. Licha ya kufanya jinai na ukatili wote huo, lakini utawala wa Kizayuni unajifanya ni wa watu waliodhulumiwa mno duniani. Hata hivyo, walimwengu wameshagundua ulaghai wa Israel na hivi sasa jamii ya kimataifa na taasisi za nchi mbalimbali zimekuwa zikichukua misimamo ya kuulaani na kuupinga waziwazi utawala huo pandikizi. Kutolewa maazimio mengi yaliyo dhidi ya utawala wa Kizayuni katika Baraza Kuu na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na misimamo ya wazi ya taasisi nyingine tofauti za umoja huo dhidi ya Israel, kuna taathira kubwa kwa walimwengu na katika maamuzi ya nchi na taasisi nyinginezo duniani.

Ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba, uamuzi wa Kamishna Mkuu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ambaye katika ripoti yake mpya amezitaka nchi zote duniani kususia kufanya biashara na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, ni uthibitisho kuwa Umoja wa Mataifa unaunga mkono harakati ya kimataifa ya kuisusia Israel.

Juhudi za kila namna za kimataifa za kuuwekea vikwazo utawala wa Kizayuni na kuutenga kimataifa zina taathira kubwa na zimewatia woga usio na kifani viongozi wa utawala wa Kizayuni. Hivi sasa nchi nyingi duniani zinazungumzia suala la kuisusia Israel na kuuwekea vikwazo utawala wa Kizayuni. Umoja wa Mataifa nao umelazimika kusikiliza kilio hicho cha walimwengu na ndio maana unaonekana kuishinikiza Israel na kuchukua maamuzi yaliyo dhidi ya utawala wa Kizayuni.

Harakati ya kuiwekea vikwazo Israel inayojulikana kwa kifupi (BDS) inaungwa mkono na jumuiya za ushirika, makundi ya kidini na taasisi zisizo za kiserikali na serikali za wananchi kote ulimwenguni na inazidi kukua siku hadi hadi siku. Si hayo tu, lakini pia vikwazo ilivyowekewa Israel hadi hivi sasa vimekuwa na madhara makubwa ya kisiasa, kidiplomasia, kiutamaduni na kiuchumi kwa utawala huo dhalimu. Kituo cha Utafiti wa Masuala ya Kiusalama cha utawala wa Kizayuni, hivi karibuni kilitoa ripoti na kusema kuwa, Israel imepata hasara ya dola bilioni 31 kutokana na vikwazo vya miaka ya hivi karibuni vya kimataifa dhidi yake.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mkutano wa Ustawi na Biashara wa Umoja wa Mataifa (UNCTAD), uwekezaji wa mubashara wa kiuchumi wa kigeni humo Israel umepungua kwa karibu asilimia 46 katika miaka ya hivi karibuni.

Hatua ya mataifa ya dunia ya kuonesha hasira zao dhidi ya utawala wa Kizayuni inathibitisha kwamba, licha ya kupita zaidi ya miongo sita ya tangu kuanzishwa utawala pandikizi katika ardhi walizoporwa Wapalestina, lakini hadi leo hii si tu Wazayuni wameshindwa kutimiza njozi yao ya kuunda dola kuu la Israel linaloanzia Mto Nile hadi Furat, lakini pia utawala wa Kizayuni unazidi kutengwa kimataifa. Muundo wa utawala wa Kizayuni unafanana na ule wa utawala wa kibaguzi wa makaburu wa Afrika Kusini ambao hatimaye umefutika katika uso wa dunia. Hatima ya utawala wa Kizayuni wa Israel nayo inaonekana wazi kuwa ni hiyo hiyo ya utawala wa ubaguzi wa rangi wa makaburu wa Afrika Kusini.