Mar 14, 2017 06:55 UTC
  • Merkel ajibu tuhuma zilizoelekezwa kwake na Erdogan

Kansela wa Ujerumani amesema kuwa, tuhuma zilizotolewa na Rais wa Uturuki dhidi yake kuhusu kuwaunga mkono magaidi hazina msingi wowote.

Steffen Seibert, msemaji wa Kansela wa Ujerumani jana alibainisha kuwa Angela Merkel hana nia ya kushiriki katika michezo ya fitina. Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki jana Jumatatu alimtuhumu Kansela wa Ujerumani Bi Angela Merkel kuwa anawaunga mkono magaidi,, anawaficha nchini kwake na kukwamisha mapambano dhidi ya ugaidi. 

Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani aliyetuhumiwa na Rais wa Uturuki kuwa anaunga mkono magaidi 

Katika siku za hivi karibuni maafisa wa miji kadhaa ya Ujerumani walifuta vikao vya uchaguzi vya maafisa wa chama tawala cha Uturuki, hatua iliyoikasirisha serikali ya Ankara. Rais wa Uturuki amelinganisha hatua hiyo ya kufutwa vikao hivyo kuwa ni sawa na hatua za utawala wa Kinazi.

Hayo yote yamejiri katika hali ambayo usiku wa Jumamosi iliyopita pia serikali ya Uholanzi ilimnyima viza ya kuingia mjini the Hague, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu na kumnyima pia kibali cha kuingia huko Rotterdam, Fatma Batul Sayan Kaya, Waziri wa Masuala ya Familia wa Uturuki. 

Mevlut Cavusoglu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ambaye amenyimwa kibali cha kuingia The Hague Uholanzi 

Itafahamika kuwa kura ya maoni ya katiba ya Uturuki itafanyika tarehe 16 mwezi Aprili na muundo wa kisiasa wa Uturuki utafanyiwa marekebisho ya kimsingi iwapo wananchi wataipigia kura ya ndiyo katiba inayopendekezwa Moja ya mabadliko hayo ni kutupilia mbali muundo wa kibunge uliopo hivi sasa na mbadala wake utakuwa ni mfumo wa utendaji wa Rais wa nchi.

Tags