Venezuela yamuita nyumbani mwanadiplomasia wake wa ngazi za juu US
(last modified Thu, 10 Mar 2016 07:57:51 GMT )
Mar 10, 2016 07:57 UTC
  • Venezuela yamuita nyumbani mwanadiplomasia wake wa ngazi za juu US

Venezuela imemuita nyumbani mwanadiplomasia wake wa ngazi za juu nchini Marekani kulalamikia hatua ya Washington ya kutangaza vikwazo vipya dhidi ya maafisa wakuu wa nchi hiyo.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amemtaka Maximilien Arvelaiz, mwanadiplomasia wa ngazi za juu wa nchi hiyo kuondoka Washington mara moja na kurejea nyumbani, huku akimkashifu vikali Rais Barack Obama wa Marekani kwa kutangaza vikwazo vipya dhidi ya maafisa 7 wa serikali ya Caracas. Katika hotuba yake hapo jana, Rais Maduro alisema Rais Obama amekuwa na fursa ya kurekebisha mgogoro wa kidipmasia kati ya pande mbili hizo lakini kwa kiburi ameamua kutangaza vikwazo vipya dhidi ya maafisa wa serikali yake. Maduro amesema taifa lake haliwezi kuvumilia jeuri na misimamo ya undumakuwili ya Washington. Amesema matamshi ya Washington kwamba Venezuela ni tishio kwa usalama wa taifa la Marekani hayakubaliki na wala hayana msingi.

Uhusiano wa kidiplomasia wa Venezuela na Marekani uliingia doa tangu mwaka 1999 baada ya hayati Hugo Chavez kuwa rais wa nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

Nchi mbili hizo hazina mabalozi wa kuziwakilisha katika miji mikuu yao tangu mwaka 2010.

Tags