Tahadhari ya Umoja wa Mataifa kuhusu maafa ya nyuklia
Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Utafiti Kuhusu Utokomezaji wa Silaha (UNIDIR) imewasilisha ripoti kamili na kutahadharisha kuwa malumbano ya kimatiafa na vita katika mitandao ya Intaneti ni jambo linaloweza kuibua maafa makubwa ya nyuklia duniani.
Ripoti hiyo, imesisitiza kuwa kumiliki silaha za nyuklia kwa msingi wa kuzuia hujuma huwa na maana tu pale wote wanapojizuia lakini iwapo zitatumika, hatari yake ni ya wazi na matokeo yake ni maafa.
Ripoti hiyo ya UNIDIR aidha imeonyesha kuwa nchi kadhaa zinaongeza bajeti ya kuunda silaha za nyuklia au kuzikarabati silaha zilizopo jambo linalopelekea kuongezeka kwa kiasi kikubwa hatari ya maafa ya nyuklia kwa makusudi au kutokusudia.
Ripoti mpya ya Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Utafiti Kuhusu Utokomezaji Silaha UNIDIR imebaini hatari ya silaha za nyuklia na muhimu zaidi ya hilo uwezekano wa kutokea vita vya nyuklia ambavyo ni tishio kwa maisha ya wanaadamu wote.
Kwa muda wa zaidi ya miaka 70 sasa dunia imekuwa ikikabiliwa na jinamizi la uwezekano wa kuibuka vita vya nyuklia na hata kumewahi kuwa na migogoro kadhaa kama ule wa makombora nchini Cuba ambao ulipelekea kukaribia vita vya nyuklia baina ya Marekani na Shirikisho la Sovieti ya zamani.
Hatari ya silaha za nyuklia inahusiana na maelfu ya silaha hizo zilizorundikwa kwenye maghala ya madola makubwa duniani na baadhi ya nchi zingine kama vile Korea Kaskazini na India ambazo nazo katika miaka ya hivi karibuni zimeweza kumiliki silaha hizo hatari.
Tokea uanze kutekelezwa Mkataba wa Kuzuia Utengenezaji na Usambazwaji Silaha za Nyuklia NPT, Umoja wa Mataifa umekuwa ukijitahidi kufanikisha suala la kuangamizwa silaha hizo.
Hii ni pamoja na kuwa mkataba huu umekuwa ukiipuuzwa na nchi nyingi hasa zenye silaha za nyuklia
Kwa hakika changamoto ya utekelezaji wa NPT inatokana na nchi zinazomiliki silaha za nyuklia kutofungamana na roho ya mkataba huo.
Mkataba wa NPT ni kwa ajili ya kudhamini kutosambazwa silaha za nyuklia duniani na pia kuchukua hatua za kivitendo katika kutokomeza silaha za nyuklia hasa zilizo katika maghala ya madola makubwa duniani.
Lakini kinyume na ilivyotarajiwa, kivitendo tumeshuhudia kuongezeka madola yaliyo na silaha za nyuklia duniani. Hivi sasa India, Korea Kaskazini, na Utawala wa Kizayuni wa Israel zimejiunga na madola makubwa duniani yenye kumiliki silaha hizo za maangamizi. Madola hayo ni wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaani Marekani, Uingereza, Ufaransa, China na Russia na yote yana idadi kubwa ya silaha hizo.
Madola hayo makubwa si tu kuwa hayaangamizi silaha zao za nyuklia bali yanaziimarisha na kuunda makombora mapya ya kurusha silaha hizo.
Kwa kuzingatia kuongezeka maghala ya silaha za nyuklia, Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Utafiti Kuhusu Utokomoezaji Silaha (UNIDIR) imeonya kuwa, kutokana na kuongezeka mifumo automatiki ya kurusha silaha za nyuklia hivi sasa kuna uwezekano mkubwa wa kuibuka vita vya nyuklia kwani mifumo hiyo automatiki inaweza kuhujumiwa kwa njia ya intaneti na kurusha kimakosa silaha hizo hatari.
Kwa kuzingatia uwezo haribifu wa silaha za nyuklia katika dunia ya leo, iwapo kutatokea vita vya nyuklia, ulimwengu utakumbwa na maafa makubwa ambayo hayajawahi kushuhidia ya kibinadamu na kimazingira.