UN yatoa wito wa kuheshimiwa uhuru wa vyombo vya habari
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuenziwa waandishi wa habari na kuheshimiwa uhuru wa vyombo vya habari.
Katika taarifa iliyotolewa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari inayoadhimishwa hii leo kote duniani, Antonio Guterres amesema: "Waandishi wa habari wanahatarisha maisha yao na kwenda sehemu hatari, ili kuwapa sauti watu wasio na sauti. Licha ya kujitolea huko, wanahabari wamekuwa wakidhalilishwa, kukandamizwa, kunajisiwa na hata kuuawa wakiwa kazini."
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa viongozi wa nchi na serikali mbalimbali duniani kutoviwekea mbinyo vyombo vya habari akisisitiza kuwa, wakati mwandishi wa habari amedhaminiwa usalama wake, maneno na picha zake zinaweza kubadilisha kabisa dunia yetu.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Waandishi Habari (IFJ), waandishi habari 93 waliuawa kwa makusudi au katika machafuko yaliyotokea kwenye maeneo mbalimbali ya dunia katika mwaka uliopita wa 2016. Mwaka 2015, waandishi habari 112 waliuawa kote duniani katika matukio mbalimbali.
Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari iliainishwa kutokana na pendekezo lililotolewa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), kwa shabaha ya kulinda na kutetea uhuru wa vyombo vya habari na kuwaenzi wadau wa sekta hiyo ambao wakati mwingine wanahatarisha maisha yao wakitekeleza wajibu na majukumu yao.