UN yaitisha mkutano wa kwanza kujadili masuala ya bahari
Umoja wa Mataifa umeandaa mkutano wa kwanza wa mambo ya baharini kuanzia tarehe 5 hadi 9 mwezi huu wa Juni, ili kubadilisha mwelekeo wa hali inayozidi kuwa mbaya ya mazingira ya ikolojia baharini, na kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu ya mambo ya bahari.
Mwenyekiti wa kikao cha 71 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Bw. Peter Thomson amesema, mkutano huo utakuwa hatua ya kwanza ya juhudi za kubadilisha hali inayozidi kuwa mbaya baharini, ili kufanikisha utekelezaji wa lengo la 14 katika ajenda ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030, la kulinda na kutumia kwa njia endelevu maliasli za baharini na kuhimiza utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu. Amesema, wakati wa ziara yake barani Afrika, ujumbe mkubwa alioupata kutoka kwa serikali na jamii za wavuvi ni kwamba wanataka mkutano huo ufanikiwe hususan katika suala la kuleta usimamizi mzuri wa hifadhi ya samaki, na kuwadhibiti wavuvi wa viwanda vikubwa wanaoingia na kumaliza samaki katika maeneo yao asili ya uvuvi.
Vile vile amegusia suala la mabadiliko ya tabianchi ambayo yatajadiliwa katika mkutano huo kuhusu bahari akisema hizo zote ni sawa na pande mbili za sarafu moja.
Kwa upande wake, naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia mambo ya uchumi na jamii Wu Hongbo ameeleza kuwa, wakati wa mkutano huo wajumbe watajadiliana uchafuzi wa mazingira ya baharini, hifadhi ya mazingira ya ikolojia ya bahari, viwanda vya uvuvi venye maendeleo endelevu na uwezo wa sayansi na utafiti kuhusu mambo ya bahari, na kutoa taarifa kuhusu mkutano huo.