Jeshi la Myanmar lapata miili na mabaki ya ndege yake iliyoanguka
(last modified Thu, 08 Jun 2017 06:49:41 GMT )
Jun 08, 2017 06:49 UTC
  • Jeshi la Myanmar lapata miili na mabaki ya ndege yake iliyoanguka

Jeshi la Myanmar limetangaza kuwa limepata mabaki ya ndege yake iliyotoweka jana Jumatano ikiwa na watu 122 katika bahari ya Andaman.

Msemaji wa timu ya habari ya jeshi hilo ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, miili kadhaa na mabaki ya ndege hiyo yamepatikana leo asubuhi saa 2 na dakika 25 kwa saa za nchi hiyo.

Kamanda Mkuu wa jeshi la Myanmar amethibitisha habari hizo katika taarifa aliyotuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook.

Ameongeza kuwa, mabaki ya ndege hiyo na makumi ya miili imepatikana katika pwani ya Launglon, kusini mwa Myanmar na kwamba ndege hiyo ilikuwa ikitokea mji wa Myeik kuelekea Yangon.

Ndege ya kijeshi ya Myanmar

Habari zinasema kuwa, nusu ya abiria waliokuwa kwenye ndege hiyo ni watu wa familia za wanajeshi, wakiwemo watoto 15, askari 35 na wahudumu 14.

Itakumbukwa kuwa, wanajeshi watano wa Myanmar walifariki dunia mwezi Februari mwaka jana, baada ya ndege yao kuripuka muda mfupi baada ya kuondoka katika uwanja wa ndege katika mji wa Naypyidaw, huku wanajeshi wengine watatu wakiaga dunia baada ya helikopta yao kuanguka na kuripuka katika maeneo ya milima mjini Bago, kusini mwa nchi, mwezi Juni mwaka huo.