Zarif: Wakuu wa Saudia wametangaza wazi wataleta vita ndani ya Iran
Waziri wa Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, "wakuu wa Saudi Arabia wametangaza wazi kuwa watahamishia vita ndani ya Iran na hili ni tishio la moja kwa moja."
Mohammad Javad Zarfi ameyasema hayo leo Jumanne mjini Oslo, Norway katika Mkutano wa Amani wa Oslo wakati akijibu swali kuhusu ni kwa nini Iran inasema Saudia imeunga mkono hujuma za kigaidi hivi karibuni Tehran. Zarif ameongeza kuwa: "Katika siku hiyo ya hujuma ya kigaidi mjini Tehran, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia Adel al Jubeir alituma ujumbe katika Twitter akisema Iran inapaswa kuadhibiwa."
Zarif alikuwa akiashiria matamshi ya Mohammad bin Salman Naibu Mrithi wa Kiti cha Ufalme na Waziri wa Ulinzi wa Saudia ambaye katika mahojiano ya hivi karibuni na televisheni rasmi ya nchi hiyo alisema: "Tunapaswa kuhamishia vita ndani ya Iran na kuibadili nchi hiyo kuwa medani ya vita."

Naye Adel al Jubeir, kabla ya mashambulio ya kigaidi Tehran Jumatano iliyopita yaliyopelekea watu 17 kuuawa shahidi na wengine 52 kujeruhiwa alikuwa ameandika ujumbe ufuatao kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter : "Iran inapaswa kuadhibiwa kwa ajili ya kuunga mkono ugaidi katika eneo."
Zarif amesema Iran imejiimarisha kiusalama na inafahamu kuwa makundi yaliyo mashariki mwa nchi yanachochewa na miezi miwili iliyopita waliua watu tisa huko Baluchistan kwa kutumia nchi jirani dhidi ya Iran.
Aidha Zarif amesema Iran inasisitiza kutatuliwa matatizo ya eneo kwa mazungumzo ya kisiasa na kuongeza kuwa Iran inataka majirani wake, hata Saudia na Qatar waishi kwa amani.