AI yakosoa vikali siasa za Marekani kuhusu wahajiri
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limekosoa vikali siasa za Rais wa Marekani kuhusu wahajiri na wakimbizi.
Taarifa iliyotolewa na Amnesty International imesema, siasa kali za serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani zimewafanya wakimbizi na wahajiri wengi watumbukie katika mitego ya magenge ya wafanya magendo ya binadamu.
Ripoti ya Amnesty International imesema baadhi ya wakimbizi wamefariki dunia wakikimbia au wakifanya jitihada za kuingia Marekani.
Afisa anayeshughulikia masuala ya America Kaskazini na Kati wa Amnesty International, Maya Liebing amesema, Donald Trump anakiuka haki za binadamu kutokana na siasa zake kali zinazohusiana na mipaka.
Miongoni mwa masuala yaliyokosolewa na Amnesty International kuhusu siasa za serikali ya Marekani ni pamoja na kuwanyima wakimbizi ruhusa ya kuingia Marekani, kuwashirikia watoto wadogo korokoroni na kutoshughulikia matakwa ya wakimbizi.
Takwimu zilizotolewa na Amnesty International zinasema kuwa, wakimbizi na wahajiri wasiopungua 71 wamepoteza maisha katika jangwa la Arizona huko Marekani katika kipindi cha kati ya Novemba 2016 hadi Aprili mwaka huu.