Kupungua imani ya kimataifa kwa Marekani ya Trump
https://parstoday.ir/sw/news/world-i31070-kupungua_imani_ya_kimataifa_kwa_marekani_ya_trump
Katika hali ambayo ni miezi mitano tu imepita tokea Donald Trump achukue usukani wa urais wa Marekani kiwango cha imani ya walimwengu kwa serikali ya nchi hiyo kimepungua sana.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 28, 2017 06:34 UTC
  • Kupungua imani ya kimataifa kwa Marekani ya Trump

Katika hali ambayo ni miezi mitano tu imepita tokea Donald Trump achukue usukani wa urais wa Marekani kiwango cha imani ya walimwengu kwa serikali ya nchi hiyo kimepungua sana.

Kituo cha utafiti cha Pew kilicho na makao makuu yake mjini Washington DC kimetangaza katika ripoti yake mpya kwamba ni asilimia 22 tu kati ya watu 40,000 waliofanyiwa mahojiano katika nchi 37 za dunia ndio walio na imani na siasa za serikali ya Donald Trump. Hii ni katika hali ambayo asilimia 60 ya walimwengu walikuwa na imani na serikali ya mtangulizi wake Barack Obama. Ni kwa kuzingatia hali hiyo ndipo ikasemekana kuwa kiwango hicho cha walimwengu kutokuwa na imani na serikali ya Marekani kilikuwa hakijawahi kushuhudiwa tena nchini humo. Kuna sababu kadhaa za kupungua kiwango hicho cha imani kwa serikali ya Trump.

Kituo cha utafiti cha Pew

Trump anachukuliwa kuwa ni nembo ya ubinafsi, kiburi na mtu asiyekubali ushuri wa viongozi wenzake katika uendeshaji wa masuala ya nchi na ya kimataifa. Trump alichukua madaraka ya nchi hiyo kupitia nara ya "Tuifanye Marekani kuwa na Nguvu Tena'' katika kampeni zake za uchaguzi na kisha kuanzisha nara nyingine ya 'Marekani Kwanza' katika siku ya kuapishwa kwake. Nara hizi zinaungwa mkono na Wamarekani waliowengi ambao wanazitazama serikali za zamani za nchi hiyo zilizokuwa zikitetea siasa za ushirikiano wa kimataifa, kama zilizokuwa zikihatarisha maslahi ya nchi hiyo. Kwa kutilia maanani suala hilo, si jambo la kushangaza kumwona Trump akijaribu kusukuma mbele waziwazi na bila ya kujali lolote, ima kwa njia za amani au kwa kutumia mabavu, siasa za kutaka kuifanya tena Marekani kuwa dola pekee lenye nguvu kubwa duniani. Ili kufikia lengo hilo, tunaona kwamba Trump amekuwa akifuatilia kwa nguvu zake zote siasa za kutuo ruzuku kubwa za kiuchumi kwa Wamarekani na daima kutunisha misuli ya nchi hiyo kwa kuishambulia Syria kwa makombora, kuitisha kijeshi Korea Kaskazini na kueneza mifarakano na fitina kati ya nchi za magharibi mwa Asia na Ghuba ya Uajemi.

Trump akiwa Riyadh Saudi Arabia kwa lengo la kuzua mifarakano na fitina kati ya nchi za eneo

Wakati huohuo ili kuiweka Marekani katika kilelel cha uchumi wa dunia, Trump ametangaza kuiondoa nchi hiyo katika mkataba muhimu wa mazingira wa Paris, ambao unaathiri moja kwa moja mustakbali wa watu bilioni sita duniani na vilevile kuhatarisha maisha ya kizazi kijacho cha wanadamu. Hata hivyo watawala wa Marekani wakiongozwa na Donald Trump wanafanya juhudi kubwa za kuirejesha Marekani katika kipindi cha dhahabu ambapo ilikuwa ikitawala dunia bila ya kuwepo upinzani wowte, huku wakiwa wameghafilika na ukweli kwamba dunia ya sasa kinyume na ilivyokuwa dunia ya kipindi cha vita baridi ambayo ilifuatiwa na kusambaratika Kambi ya Mashariki, haiko tayari tena kukubali kuongozwa na kambi moja tu yenye nguvu ya Marekani. Dunia ya leo kinyume na ilivyokuwa huko nyuma, inapendelea kuona kukiwepo nguvu kadhaa zilizo na sera tofauti.  Kwa sasa kuna nguvu mpya kadhaa zilizodhihiri katika uwanja wa uchumi na mataumizi ya zana za kivita yamepungua kwa kiwango kikubwa.

Askari wa Marekani wakichochea moto wa vita Mashariki ya Kati

Kuhusiana na hilo, watu wengi duniani wana ufahamu mzuri kuhusu mambo yanayoendelea ulimwenguni na wanafahamu kwa kina athari mbaya zinazotokana na ubeberu na matumizi mabaya ya silala. Kwa msingi huo na kinyume na ilivyokuwa katika nusu ya pili ya karne iliyopita ambapo Marekani ilifanikiwa kudhibiti karibu nusu ya ulimwengu kupitia vitisho na vishawishi, hivi sasa imeshindwa kabisa kuhuisha hali hiyo ambapo hata imeshindwa kuzishawishi nchi rafiki zake za karibu kushirikiana nayo katika kufanikisha lengo hilo. Kuharibika kwa sifa za serikali ya nchi hiyo mbele ya fikra za waliowengi duniani, kumepunguza kwa kiwango kikubwa na kimataifa ushawishi wake wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni, jambo ambalo linatajwa na wengi kuwa mwanzo wa kudhoofika na hatimaye kusambaratika nchi hiyo.