Maandamano dhidi ya marufuku ya Trump kwa wahajiri yafanyika Marekani
Wananchi wa Marekani wanaopinga utekelezaji wa amri iliyotolewa na Rais Donald Trump wa nchi hiyo inayowapiga marufuku raia wa nchi sita zenye idadi kubwa ya Waislamu kuingia Marekani, waliandamana jana katika mitaa ya New York na Los Angeles.
Waandamanaji hao wametaka kusitishwa marufuku hiyo haraka iwezekanavyo.
Wakati huo huo mawakili na wanaharakati wa kutetea haki za wahajiri jana walikwenda katika uwanja wa ndege wa John F. Kennedy mjini New York ili kutoa msaada wa kisheria kwa mtu yoyote ambaye anatatizwa na amri hiyo ya Trump. Waandamanaji hao katika miji ya New York na Los Angeles walisema kuwa amri hiyo ya marufuku ni ya kibaguzi, na kwamba haiwezi kuzidisha usalama wa Marekani.
Wamesema hatua ya Donald Trump ya kuwapiga marufuku Waislamu wa nchi sita kuingia Marekani ni kitendo cha kibaguzi, chenye kuzusha chuki na kilicho kinyume na thamani za nchi hiyo.
Sehemu ya amri hiyo ya marufuku ya Trump ilianza kutekelezwa jana Alhamisi kufuatia mwafaka wa Mahakama Kuu ya Marekani. Balozi na balozi ndogo za Marekani pia zimeanza kuzuia utoaji wa viza kwa raia wa nchi zilizotajwa kwa muda wa siku 90 kwa mujibu wa amri hiyo.