Nigeria yazitaka nchi za G20 kutekeleza majukumu yao kuhusu Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/world-i31502-nigeria_yazitaka_nchi_za_g20_kutekeleza_majukumu_yao_kuhusu_afrika
Nigeria imezitaka nchi wanachama katika kundi maarufu kwa jina la G20 kutekeleza majukumu yao kuhusu bara la Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 08, 2017 11:35 UTC
  • Nigeria yazitaka nchi za G20 kutekeleza majukumu yao kuhusu Afrika

Nigeria imezitaka nchi wanachama katika kundi maarufu kwa jina la G20 kutekeleza majukumu yao kuhusu bara la Afrika.

Makamu wa Rais wa Nigeria, Yemi Osinbajo amewataka viongozi wa nchi za Ulaya kuchukua hatua za kivitendo za kutekeleza majukumu yao kuhusu bara la Afika na amemshukuru Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ambaye ndiye mwenyekiti wa sasa wa kundi hilo kwa kulipa kipaumbele suala la ustawi na maendeleo ya Afrika. 

Yemi Osinbajo amesema kuwa, sasa ni wakati wa kutekelezwa ahadi na majukumu ya washirika wa Afika wa bara Ulaya na kwamba Afrika iko tayari kukabiliana na kuyashinda matatizo na vizingiti vinavyokwamisha ustawi na maendeleo ya watu wake. 

Mkutano wa G20, Ujerumani

Makamu wa Rais wa Nigeria amesema, sambamba na kukamilika mipango ya Umoja wa Ulaya katika uwanja wa kupambana na utakatishaji wa fedha, nchi za Ufaransa, Ujerumani, Italia na Uingereza ambazo ndio nguzo kuu ya G20, zinaweza kutumia fursa hiyo kwa ajili ya kulisaidia bara la Afrika katika uwanja huo. 

Nchi za Afrika ambazo kila mwaka hupoteza zaidi ya dola bilioni 50 katika miamala isiyo halali ya kifedha, mwaka jana wa 2016 zilianzisha jitihada za kurejesha mabilioni ya dola zilizoibwa barani humo na kupelekwa Ulaya.