Maduro: CIA inashirikiana na Mexico, Colombia dhidi ya Venezuela
(last modified Tue, 25 Jul 2017 14:13:08 GMT )
Jul 25, 2017 14:13 UTC
  • Maduro: CIA inashirikiana na Mexico, Colombia dhidi ya Venezuela

Rais wa Venezuela amesema Shirika la Kijasusi la Marekani CIA linashirikiana na Mexico na Colombia katika njama ya kuipindua serikali halali ya Caracas.

Nicolas Maduro amesema serikali za nchi hizo mbili jirani zake, yaani Colombia na Mexico inafaa zitoe ufafanuzi kuhusu matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Mkurugenzi wa CIA, Mike Pompeo, aliyesema kuwa amefanya mazungumzo na viongozi wa serikali za Mexico City na Bogota kuhusu kadhia ya Venezuela.

Rais wa Venezuela amebainisha kuwa, Mexico na Colombia zinashirikiana na Marekani ili kulinda maslahi yao ya mafuta.

Tangu mwezi Aprili mwaka huu, Venezuela imekuwa ikishuhudia maandamano ya waungaji mkono na wapinzani wa serikali, ambapo hadi sasa makumi ya watu wameuawa katika vurumai hizo.

Maandamano mjini Caracas

Uadui wa Marekani dhidi ya Venezuela hujaanza sasa katika wa utawala wa Rais Donald Trump, ambaye mwezi Februari mwaka huu, siku chache baada ya kuapishwa, alikutana na mke wa Leopoldo López, kiongozi mkuu wa upinzani anayezuiliwa katika jela nchini Venezuela.

Mwezi Machi mwaka 2015 rais wa zamani wa Marekani Barack Obama alitoa amri ya utekelezaji wa vikwazo dhidi ya Caracas, ambapo aliitaja Venezuela kuwa tishio kwa uslama wa taifa la Marekani.

Tangu alipoingia madarakani hayati Hugo Chávez, rais wa zamani wa nchi hiyo, Marekani imekuwa ikitekeleza siasa za uhasama dhidi ya viongozi wa Venezuela.

Tags