Putin: Kuishinikiza Korea ya Kaskazini hakutakuwa na taathira
Rais Vladimir Putin wa Russia ameishauri Marekani na waitifaki wake barani Asia kutochukua hatua za kuishinikiza Korea ya Kaskazini na ametoa wito wa mazungumzo ili kuhitimisha mvutano kuhusu miradi ya silaha za nyuklia za nchi hiyo.
Putin ameandika katika makala iliyotolewa jana na ikulu ya Kremlin kwamba, sera za kuishinikiza Korea ya Kaskazini ili isitishe miradi yake ya makombora ya nyuklia zimepotoka na hazina maana.

Amesema matatizo ya Peninsula ya Korea yanapasa kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya kufanya mazungumzo ya pande zote husika bila ya masharti yoyote. Amesema kauli za mabavu na vitisho, mashinikizo na matumizi ya nguvu za kijeshi hazina maana yoyote.
Rais Vladimir Putin wqa Russia amesema nchi yake na China tayari zimeandaa ramani ya njia ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Peninsula ya Korea, ambayo imebuniwa kwa lengo la kupunguza hali ya mivutano na kuanzisha fremu itakayopelekea kupatikana amani ya kudumu. Ameongeza kuwa, ramani hiyo ya njia inazuia kutumiwa vitisho na nguvu ya aina yoyote na inasisitiza kutumia njia za kisiasa na kidiplomasia kutatua matatizo yote katika eneo hilo.