Erdogan afichua jinsi NATO inavyowasaidia magaidi wa ISIS
https://parstoday.ir/sw/news/world-i33854-erdogan_afichua_jinsi_nato_inavyowasaidia_magaidi_wa_isis
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amefichua kwamba nchi moja mwanachama wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi NATO ndiye mhusika wakuu wa kuwatumia silaha magaidi wa Daesh yaani ÏSIS.
(last modified 2026-05-13T18:57:29+00:00 )
Sep 01, 2017 09:35 UTC
  • Erdogan afichua jinsi NATO inavyowasaidia magaidi wa ISIS

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amefichua kwamba nchi moja mwanachama wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi NATO ndiye mhusika wakuu wa kuwatumia silaha magaidi wa Daesh yaani ÏSIS.

Ijapokuwa Erdogan hakutaja kwa jina nchi yoyote ile, lakini ni jambo lisilo na shaka kwamba kati ya nchi wanachama wa NATO, Marekani ndiyo iliyoko mstari wa mbele katika kuyasaidia kwa kila namna magenge ya kigaidi hususan ISIS.

Uhakika huo ulibainishwa wazi katika majukwaa ya mikutano ya hadhara ya kampeni za uchaguzi wa hivi karibuni wa rais nchini Marekani, wakati wagombea wa vyama viwili vya Republican na Democrats Donald Trump na Hillary Clinton walipokuwa wanaumbuana majukwaani. Uhakika huo ulifichuliwa pia katika mijadala ya moja kwa moja ya uchaguzi iliyofanyika kati ya wagombea hao wawili. 

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki 

 

Kabla ya hapo pia, Hillary Clinton, waziri wa mambo ya nje wa zamani wa Marekani alikuwa amekiri kwamba nchi yake ndiyo iliyounda genge la kigaidi la Daesh kwa ajili ya kuuvuruga Uislamu na kulinda kile kilichodaiwa na Clinton kuwa ni maslahi ya Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati. 

Ni jambo lisilo na shaka hata kidogo kwamba Marekani ndiye muungaji mkuu wa magenge ya kigaidi duniani. Ni nchi ambayo kwa misimamo yake ya kibeberu,  inachochea maafa na mauaji katika kona mbalimbali za dunia hususan Mashariki ya Kati ili kufanikisha malengo yake haramu.

Kiujumla kumezungumzwa mengi kuhusiana na misaada ya kifedha na kisilaha inayotumwa kwa magaidi wanaofanya jinai katika nchi kama Syria na Iraq. Wachambuzi wengi wa mambo, wasomi, wanafikra na waandishi wa habari muda wote wamekuwa wakifuatilia suala hilo.

Magaidi wa ISIS wakijiandaa kufanya jinai nchini Syria

 

Miongoni mwa ushahidi uliotolewa kuhusiana na suala hilo ni ule uliosambazwa na Dilyana Gaytandzhieva, mwandishi wa habari wa zamani wa gazeti la Trud linalochapishwa Sofia, mji mkuu wa Bulgaria. Mwandishi huyo alifichua jinsi Marekani na utawala wa Israel pamoja na Saudi Arabia na Imarati zinavyoendesha mpango wa siri wa kuwafikishia silaha magaidi wa Daesh na al Qaida kwa usimamizi kamili wa Shirika la Kijasusi la Marekani CIA.

Gazeti la Trud la Bulgaria lilimfuta kazi mara moja Bi Dilyana Gaytandzhieva baada tu ya kusambaza habari hiyo ya kufichua uhalisia wa mambo kuhusu magenge ya kigaidi duniani kama vile Daesh na jinsi nchi kama Marekani, Saudia, Umoja wa Falme za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel zinavyohusika moja kwa moja katika kuyapa silaha magenge hayo.

Ripoti ya mwandishi huyo ilisema pia kwamba serikali ya Rais Ilham Aliyev wa Azerbaijan ilihusika kwenye njama hizo. Mwandishi huyo wa habari wa Bulgaria anasema:

Ndege zisizopungua 350 za kidiplomasia zilitumika kutuma silaha katika maeneo tofauti yenye vita duniani katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Ndege za serikali ya Rais Ilham Aliyev wa Azerbaijan ziliwapelekea magaidi kiwango kikubwa cha silaha za kila namna, nyepesi na nzito kupitia safari za kidiplomasia.

Vile vile amesema: Shirika la Ndege la serikali ya Azerbaijan linalojulikana kwa jina la Silk Way Airlines lilitumia ndege zake kwa msaada wa Israel, Marekani, Saudia na Imarati kuwafikishia silaha magaidi.

Dilyana Gaytandzhieva, mwandishi wa habari wa Bulgaria aliyefutwa kazi kwa kufichua namna nchi za Magharibi na Saudia na Imarati zinavyowatumia silaha magaidi wa ISIS

 

Amma jambo lisilo na shaka hata kidogo hapa ni kwamba, serikali ya Uturuki nayo iko katika safu ya mbele ya nchi ambazo zimetoa mchango mkubwa wa kupata nguvu magenge ya kigaidi hususan ISIS. Kwa kweli Rais wa Uturuki amefichua uhakika huo mchungu wa jinsi Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi NATO ulivyo na mchango mkubwa katika kuwafikia silaha magaidi kwenye nchi kama Syria na Iraq katika hali ambayo serikali za Damascus na Baghdad mara kwa mara zimekuwa zikiilaumu vikali serikali ya Uturuki kwa kuhusika katika mauaji ya watu wasio na hatia na raia wa kawaida wa Syria na Iraq.