Sep 02, 2017 07:42 UTC
  • Erdogan: Mauaji ya Waislamu wa Warohingya ni ya kimbari

Rais wa Uturuki Recep Teyyip Erdogan ameyataja mauaji ya mamia ya Waislamu wa kabila la Rohingya huko Myanmar kama mauaji ya kimbari.

Akiongea hapo jana mjini Istanbul, Erdogan amesema kama tunavyomnukuu: "Kuna mauaji ya kimbari huko Rakhine, lakini ulimwengu umeamua kuyafumbia macho." Mwisho wa kunukuu.

Amesema mauaji hayo yanayofanyika nyuma ya pazia la demokrasia ni ya kusikitisha na kwamba vyombo vyote husika vya kimataifa vinavyoyapuuza vinabeba dhima.

Rais wa Uturuki amesema kadhia hiyo itajadiliwa kwa kina katika mkutano ujao wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katikati ya mwezi huu wa Septemba mjini New York.

Nyumba za Waislamu wa Rohingya zilizoteketezwa moto

Takwimu ramsi zinaonyesha kuwa watu 400 wamepoteza maisha katika jimbo la Rakhine tokea Ijumaa iliyopita hadi sasa. Kati ya walipooteza maisha ni wale waliouliwa na jeshi la nchi hiyo katika oparesheni  dhidi ya Waislamu huku makumi ya wengine wakiwemo wanawake na watoto wadogo, wakipoteza maisha wakati wakivuka mto kukimbia mapigano katika jimbo la Rakhine.

Maelfu ya Waislamu wa Myanmar wamekimbilia nchini Bangladesh wakihofia jinai zaidi za wanajeshi wa nchi hiyo na Mabudha wenye misimamo mikali dhidi yao.

 

Tags