UN yataka Korea Kaskazini isitishe majaribio ya nyuklia
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali jaribio la nyuklia lililofanywa Jumapili na Korea Kaskazini.
Jaribio hilo lililofanyiwa chini ya ardhi, ni la sita tangu mwaka 2006 na linafuatia majaribio mengine mawili ya aina hiyo yaliyofanywa mwaka jana.
Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemnukuu Katibu Mkuu akisema kuwa kitendo hicho cha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, DPRK, (Jina rasmi la Korea Kaskazini) ni ukiukwaji mkubwa wa wajibu wa nchi hiyo kimataifa na kinadumaza jitihada za kimataifa za kuondokana na uenezaji na usambazaji wa silaha.
Bwana Guterres amesema DPRK pia inaendelea kukiuka maadili ya kimataifa kuhusu majaribio ya nyuklia akisema anafuatilia kwa karibu hali ya sasa huku akishauriana na pande husika.
Nao Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, IAEA umetoa taarifa na kusema unafuatilia kwa karibu mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini na uko tayari kuchangia katika ufumbuzi wa amani wa mgogoro wa Peninsula ya Korea.
Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Yukia Amano ameitaka DPRK itekeleze maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na IAEA.
Korea Kaskazini jana ilitangaza kufanyia majaribio kwa mafanikio bomu la nyuklia, ambalo limesababisha mtetemeko wa ardhi uliokuwa na ukubwa wa 6.3 kwa kipimo cha rishta.
Pyongyang imefanya jaribio hilo licha ya taharuki kutanda katika Peninsula ya Korea na vikwazo vya kila mara vya Marekani na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi yake.