Tillerson: Chaguo la kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini liko mezani
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa, chaguo la kijeshi la Washington dhidi ya Korea ya Kaskazini bado liko mezani.
Rex Tillerson amesema kuwa Washington inafikiria pia kutumia udiplomasia katika kukabiliana na Pyongyang. Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Tillerson amesema kuhusiana na Russia kwamba: Washington itaendelea kushirikiana na Moscow kuhusu masuala ya kimataifa licha ya kuwepo hitilafu kubwa katika uhusiano pande hizo mbili.
Rais Donald Trump wa Marekani pia ametuma ujumbe katika mtandao wa twitter akimtaja Kim Jong -un, kiongozi wa Korea Kaskazini kuwa ni kichaa na kutishia kwamba Korea Kaskazini itakabilwia na majaribio ambayo haijawahi kukutana nayo hapo awali."
Juzi Alhamisi Rais Donald Trump wa Marekani alisema kuwa ataiwekea Pyongyang vikwazo zaidi.
Mvutano kati ya Marekani na Korea Kaskazini umeshika kasi katika siku za hivi karibuni huku Rais Donald Trump akidhihirisha azma ya kutaka kuanzisha vita dhidi ya nchi hiyo. Pyongyang kwa upande wake imetishia kuwa italifanyia majaribio bomu la haydrogen katika bahari ya Pacific.