Marekani yajiondoa katika Mkataba wa Kimataifa wa Uhamiaji
Serikali ya Marekani imetangaza kuwa, nchi hiyo imejiondoa katika Mkataba wa Kimataifa wa Uhamiaji unaoshughulikia masuala ya kuboresha na kusimamia masuala ya wahajiri na wakimbizi.
Uamuzi huo ni mfano wa karibuni zaidi wa upinzani wa serikali ya Donald Trump dhidi ya mikataba na makubaliano ya kimataifa tena kuhusu maudhui ya kukabiliana na athari mbaya za uhamiaji katika upeo wa kimataifa.
Ofisi ya mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa imedai kuwa, mkataba uliotiwa saini mwaka 2016 na kupasishwa na nchi 193 wanachama wa umoja huo haudhamini maslahi ya Marekani na siasa za uhamiaji za serikali ya nchi hiyo. Katika mkataba huo uliopewa jina la New York Declaration for Refugees and Migrants, nchi zilizotia saini mkataba huo zinalazimika kuheshimu haki za wakimbizi, kuwatayarishia makazi na kuwawezesha kupata elimu na kazi. Majukumu haya yanakinzana na sera zinazopiga vita wakimbizi na wahajiri za Rais Donald Trump wa Marekani na kwa msingi huo White House imeendeleza mwenendo wake wa kujiondoa katika mikataba na makubaliano ya kikanda na kimataifa kwa kutoa tangazo la kujionda katika mkataba huo unaojulikana kama Azimio la New York.
Kabla ya hapo Marekani ilikuwa tayari imetangaza kujiondoa katika makubaliano ya Trans-Pacific, mkataba wa hali ya hewa wa Paris na shirika la UNESCO. Sasa ni zamu ya kuhujumu mkataba wa wahajiri na wakimbizi unaoshambuliwa na kupigwa kalamu nyekundu na serikali ya Trump kwa kutumia kaulimbiu ya “Marekani Kwanza”. Kabla ya hatua hiyo Trump alikuwa tayari ametoa maagizo ya kufutwa sheria kadhaa zinazowalinda wakimbizi na wahajiri na hata watu walioomba viza za kuingia nchini Marekani. Hivyo kujiondoa kwa Marekani katika mkataba wa Azimio la New York ni sawa na kutekeleza upande wa kimataifa wa sera za kuwapiga vita wahajiri na wakimbizi za serikali ya Donald Trump.
Pamoja na hayo ofisi ya mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa imedai kuwa, nchi hiyo itaendelea kuwahami wakimbizi na wahajiri na wale wanaoomba hifadhi. Hata hivyo mwenendo wa karibu mwaka mmoja uliopita wa ikulu ya Rais wa Marekani umeonesha kuwa, nchi hiyo haitaki tena kuwasaidia wakimbizi na watu wanaoomba hifadhi. Hii ni licha ya kuwa, Marekani imejengwa na wahajiri na wakimbizi ambao walivumilia mashaka mengi nchini Marekani na matatizo ya kuwa mbali na nchi zao za asili kwa ajili ya kupata maisha bora.
Kwa mujibu wa mtazamo wa wazungu wabaguzi wa rangi ambao Trump ni mwakilishi wa mitazamo na fikra zao, wahajiri na wakimbizi ni watu wanaosababisha matatizo ambao hawapaswi kuruhusiwa kukanyaga ardhi ya Marekani. Katika upande mwingine wafuasi wa mrengo wa kulia wa Marekani hawafurahishwi kuona kuwa, masuala na sera za uhajiri yanadhibitiwa na kupangwa na taasisi za kimataifa. Kundi hilo linaamini kuwa, maslahi ya Marekani yanapaswa kutangulizwa mbele ya kila kitu na pale sheria za kimataifa zinapopingana na maslahi ya nchi hiyo, basi Washington inapaswa kujiondoa mara moja katika makubaliano na mikataba ya kimataifa hata kama italazimu kuharibiwa au kukanyagwa hatima ya maelfu ya wahajiri na watu waliokimbia vita, machafuko na makucha ya balaa la njaa.
Sera hizi za serikali ya Donald Trump zinazidisha mara dufu mashaka na matatizo na wahajiri na wakimbizi.