Marekani yatoa vitisho tena vya kuishambulia kijeshi Korea Kaskazini
https://parstoday.ir/sw/news/world-i37665-marekani_yatoa_vitisho_tena_vya_kuishambulia_kijeshi_korea_kaskazini
Katika kile kinachoonekana kama jaribio la kuilazimisha Korea Kaskazini iachane na mipango yake ya makombora na ya kinyuklia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson ametoa vitisho tena kwa lugha isiyo ya wazi vya kuishambulia kijeshi nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 16, 2017 07:58 UTC
  • Marekani yatoa vitisho tena vya kuishambulia kijeshi Korea Kaskazini

Katika kile kinachoonekana kama jaribio la kuilazimisha Korea Kaskazini iachane na mipango yake ya makombora na ya kinyuklia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson ametoa vitisho tena kwa lugha isiyo ya wazi vya kuishambulia kijeshi nchi hiyo.

Akihutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa cha kujadili mipango ya nyuklia na makombora ya Korea Kaskazini, Tillerson amesema nchi hiyo ndiye adui mkubwa zaidi wa Marekani na kuongeza kwamba ana matumaini utatuzi wa kadhia ya mipango ya nyuklia na makombora ya Pyongyang utapatikana kwa njia za kidiplomasia badala ya kuishia kwenye vita.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ameongeza kuwa kabla ya kuanza mazungumzo kati ya Washington na Pyongyang, Korea Kaskazini inapaswa kusimamisha kwanza shughuli zake za nyuklia na za kijeshi.

Aidha amesema Marekani imefanya kila ilichoweza ili kusimamisha mipango ya nyuklia na makombora ya Korea Kaskazini.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson (kulia) na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un

Matamshi hayo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani yanatolewa katika hali ambayo, Ikulu ya White House imetangaza mara kadhaa kuwa msimamo wa Washington kuhusu Pyongyang bado haujabadilika na kwamba Marekani itaendelea kutoa mashinikizo ya kijeshi na kiuchumi na kuiwekea vikwazo Korea Kaskazini.

Marekani, ambayo ina nafasi kubwa katika kukoleza moto wa mivutano kwenye eneo la Peninsula ya Korea imekuwa kila mara ikishikilia Korea Kaskazini isimamishe majaribio yake ya nyuklia, lakini viongozi wa Pyongyang wanasisitiza kwamba madamu Marekani na waitifaki wake wanaendelea kutoa vitisho dhidi ya Korea Kaskazini, nchi hiyo nayo itaendelea kujiimarisha kijeshi.../